Waziri wa Fedha na Mpango Mhe.Dr.Philip Mpango akiwaonyesha waandishi wa
Habari mkoba wenye hotuba ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018 leo Bungeni
Mjini Dodoma tarehe 8th June 2018.
Wabunge wakiingia Ukumbi wa Bunge kusikiliza hotuba ya bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2017/2018 leo Bungeni Mjini Dodoma tarehe 8th June 2018.
Kasi ya ukuaji wa uchumi nchini imeendelea kuimarika
ambapo Tanzania imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika zilizoongoza kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa
uchumi.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka 2017/2018
bungeni leo, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema kuwa kwa
mujibu wa takwimu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF),
Tanzania inashika nafasi ya pili kwa ukuaji wa
uchumi ambapo uchumi wake unakuwa kwa asilimia 7.1 nyuma ya Ivory Coast ambayo
yenyewe uchumi wake unakuwa kwa asilimia 7.9.
Nchi zingine zilizokuwa na
kasi nzuri ya ukuaji wa uchumi ni Senegal (asilimia 6.6), Djibouti (asilimia
6.5) na Ethiopia (asilimia 6.5).
“Jarida
la Benki ya Dunia (Tanzania Economic Update) lililochapishwa Aprili 2017
linabainisha waziwazi kuwa uchumi wa Taifa ni imara kwa kuangalia viashiria
mbalimbali kama ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei, urari wa biashara, akiba
katika fedha za kigeni na thamani ya shilingi”. Alieleza Waziri Mpango kwa
kunukuu takwimu za Benki ya Dunia juu ya ukuaji wa uchumi nchini.
Alisema kuwa pamoja
na mafanikio yaliyoelezwa lakini bado kumekuwa na mijadala kuhusu afya ya
uchumi wa Taifa hususan ukwasi katika uchumi, kufungwa kwa biashara, na madai
kwamba sekta binafsi imepoteza matumaini na kujiamini (private sector
confidence) na kwamba hali hiyo imesababishwa
na mambo mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa mikopo chefuchefu katika mabenki.
“Takwimu pia zinaonesha kuwa ukwasi wa
mabenki ulianza kutetereka kutokana na kuongezeka kwa mikopo chefuchefu kutoka
asilimia 8.3 mwezi Machi 2016 hadi asilimia 10.9 Machi 2017 ikilinganishwa na
kiwango kinachohitajika cha asilimia 5.
Alifafanua kuwa Mikopo kwa sekta binafsi
iliongezeka kidogo kwa asilimia 3.7 katika kipindi cha mwaka ulioishia Machi
2017 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 23.6 katika kipindi kama hicho
mwaka 2016.
“Kupungua kwa kiwango cha ukuaji huo
kulitokana kwa kiasi kikubwa na kuyumba kwa biashara duniani ambako kuliathiri
nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania”. Alifafanua Dkt. Mpango.
Aidha katika bajeti hiyo, aliyataka mabenki
yote nchini kusimamia kwa makini taratibu za kibenki katika utoaji wa mikopo.
Alieleza kuwa ili kuimarisha ukwasi,
Serikali kupitia Benki Kuu imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kupunguza riba ambazo benki za biashara hukopa kutoka Benki Kuu (Discount Rate)
ili kuongeza ukwasi katika benki za biashara
na hivyo kuziwezesha kukopa kwa gharama nafuu zaidi.
Kwa mujibu wa Waziri Mpango, riba hiyo
imepunguzwa kutoka asilimia 16.0 iliyokuwa ikitumika tangu mwezi Novemba 2013
hadi asilimia 12.0 ambayo imeanza kutumika rasmi tarehe 6 Machi 2017.
Aidha, ameeleza kuwa katika kuimarisha
zaidi soko la fedha nchini, Benki Kuu ilipunguza kiwango cha amana ambacho
benki za biashara zinatakiwa kuhifadhi Benki kuu kama dhamana (Statutory
Minimum Reserve Requirement – SMR) kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0 ili
kuziwezesha benki za biashara kuwa na ukwasi zaidi kwa ajili ya kukopesha sekta
binafsi na kwamba hatua hiyo imeanza kutumika rasmi mwezi Aprili 2017..
“Ni matumaini ya Serikali kuwa hatua hizi
zitaziwezesha benki za biashara nchini kuongeza ukwasi wa kutosha kuwakopesha
wananchi kwa riba nafuu”. Alieleza.
Katika eneo la mazingira ya kufanya biashara, Waziri
mpango alieleza kuwa Serikali imeanza kuona
viashiria bora zaidi katika eneo la kuboresha mazingira ya biashara.
Amesema kwa mujibu wa taarifa
ya Benki ya Dunia ya mwaka 2017 ilionesha kuwa, Tanzania ilikuwa nchi ya 132
kwa urahisi wa kufanya biashara ikiwa imepiga hatua kwa nafasi 12 kutoka nafasi
ya 144 mwaka 2016.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa
ya “Fahirisi ya Uwekezaji Afrika ya mwaka 2016” (Africa Investment Index, 2016)
iliyotolewa na taasisi ya “Quantum Global
Research Lab” ya Uingereza, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza miongoni mwa
nchi za Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji na ya nane kwa Afrika, ikiwa
imepiga hatua kutoka nafasi ya 19 mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment