Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli aahidi nyongeza ya kawaida kwa mishahara na kuwapandisha
madaraja wafanyakazi wanaostahili.
Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo leo alipokuwa mgeni
rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo Kitaifa
yamefanyika katika viwanja vya Chuo Cha Ushirika, Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Dkt. Magufuli alisema Serikali ilisitisha upandishaji
wa vyeo na mishahara kutokana na kuwepo na watumishi hewa na walioghushi vyeti
lakini baada ya kuondolewa Serikali itahakikisha inashughulikia maslahi ya wafanyakazi.
“Watumishi 9932 walikuwa na vyeti feki,watumishi
hewa walikuwa 19706 hivyo kama Serikali ingeongeza mishahara inamaana watumishi
hawa pia wangefaidika na pesa ambazo hawakustahili kuzipata”, alisema Dkt.
Magufuli.
Aidha aliwataka waajiri kuheshimu na kutoa mikataba
ya kazi na kutowanyanyasa wafanya kazi wao na wafanyakazi kuomba kazi kulingana
na elimu zao na waache tabia ya kughushi vyeti.
Aliongeza kuwa Serikali itashughulikia mfumuko wa
bei za bidhaa na kuhakikisha viwanda vingi vitajengwa sehemu mbalimbali nchini
ili kuongeza ajira kwa vijana wa kitanzania.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TUCTA Dkt. Yahya
Msigwa ameipongeza Serikali kwa kutekeleza ahadi zake na kuopngeza kuwa hiyo ni
ishara tosha kuwa Serikali inayodhamira ya dhati ya kuwajali wananchi wake
wakiwemo wafanyakazi.
Ameongeza kuwa wanayo imani kubwa kwa Serikali kuwa
itatekeleza ahadi yake ya kufanyia maboresho ya maslahi ya umma kama ambavyo
umeonyesha nia njema ya kutekeleza ahadi zake.
Alizitaja baadhi ya ahadi zilizotekelezwa kuwa ni
pamoja, kupiga vita rushwa na ufisadi, kuondoa watumishi hewa, Serikali kuhamia
Dodoma, ujenzi wa miundombinu ya reli, vita dhidi ya dawa za kulevya pamoja na
ununuzi wa ndege.
“Ni imani yetu kuwa ahadi hii ya kuboresha maslahi
kwa Watumishi wa Umma itatekelezwa kwa wakati kwani tayari umekwisha ondoa
mambo yaliyokuwa yanakwamisha zoezi hilo,” alisema Dkt. Msigwa.
Wakati huohuo Katibu Mkuu huyo ameiomba Serikali
kuharakisha kubuni namna ambavyo wafanyakazi watanufaika na Mifuko ya Jamii na
wanaodai mapato yao kusikilizwa kesi zao kwa wakati.
Maadhimisho hayo yameuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa Kitaifa akiwemo Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Job Ndugai,Naibu Spika Tulia Ackson,
Mawaziri Jenister Mhagama na Angella Kairuki, Profesa Jumanne Maghembe na
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi pamoja na baadhi ya Wabunge. Kauli mbiu
ya maadhimisho hayo ni “Uchumi wa Viwanda Vizingatie Haki, Maslahi
na Heshima ya Mfanyakazi”.
No comments:
Post a Comment