Tuesday, 16 May 2017

SERIKALI IMEKUSANYA BILIONI 63 KUPITIA MTAMBO WA KUHAKIKI NA KUSIMAMIA HUDUMA ZA MAWASILIANO YA SIMU NCHINI



Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) imekusanya shilingi bilioni 63,015,450,230 kwa kipindi cha Octoba 2013 mpaka Februari 2017 tangu kuanzishwa kwa mtambo wa kuhakiki na kusimamia Huduma za Mawasiliano(TTMS) nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe.Edwin Ngonyani wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigamboni Mhe.Dkt Faustine Engelbert leo Bungeni.

“Mtambo huu umesaidia Mamlaka ya Mawasiliano nchini kuongeza ufanisi katika kusimamia Sekta ya Mawasiliano pamoja na kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko yanayotokea katika Sekta ya Mawasiliano Duniani kote”,Aliongeza Mhe.Ngonyani

Aidha kati ya pesa izo bilioni 56,987,368,631 zimewasilishwa hazina na shilingi bilioni 6,028,081,599 zimewasilishwa Tume ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH) kwa ajili ya kugharamia tafiti mbalimbali zenye manufaa kwa nchi yetu ambapo kabla ya hapo kahukuwa na mapato hayo.

Amesema mtambo huu umeiwezesha TCRA kuwa na uwezo wa kusimamia mawasiliano ya simu za Kimataifa na zile za mwingiliano,pia mtambo huo umesaidia kudhibiti mawasiliano ya Simu za ulaghai za kimataifa na kusimamia ubora wa mitandao katika kutoa huduma bora kwa wananchi,kudhibiti namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano nchini pamoja na usimamiaji wa miamala ya fedha  inayopita katika mitandao ya simu hapa nchini.

“Aidha pamoja na mafanikio hayo jitihada za kuboresha zaidi mfumo huu ili kuweza kubaini na kujiridhisha juu ya mapato yote yatokanayo na huduma za  mawasiliano na yanayokidhi mahitaji ya Mamlaka ya Mapato Tanzania,Benki kuu ya Tanzania na TCRA zinaendelea”Aliongeza Mhe.Ngonyani.


Aidha Serikali itaendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa TCRA ili waweze kuendana na kasi ya ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano hususani katika eneo hili la kuchakata taarifa mbalimbali za huduma za mawasiliano zinazopatikana kutoka kwa watoa huduma ili kuweza na kujiridhisha juu ya mapato yote.

No comments:

Post a Comment