Serikali kupitia
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeahidi
kushughulikia suala la huduma za afya bure kwa watu wenye ulemavu.
Hayo yamesemwa leo
Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla kwa niaba ya Waziri
Ummy Mwalimu.
Akizungumza wakati wa
kipindi cha maswali na majibu kufuatia swali la Mbunge wa Viti Maalum Stella
Ikupa Alex aliyetaka kupata ufafanuzi juu ya suala hilo, Dkt. Kigwangalla
alisema kuwa dhamira ya Serikali ni kutoa huduma za afya bure kwa makundi
maalum likiwemo watu wenye ulemavu.
“Dhumuni la Sera ya
Afya ya mwaka 2007 ni kuwezesha watu wenye ulemavu wazingatiwe katika makundi
maalum ya watu wanaostahili msamaha utolewao kwa kuzingatia endapo mlemavu huyo
hana uwezo wa kulipia huduma hiyo au awe katika makundi maalum ili kupata
huduma bora za afya kama ilivyo kwa watu wengine,” alisisitiza Dkt.Kigwangalla.
Sera hiyo
imeainisha makundi maalum yanayostahili kupata msamaha wa huduma za afya katika
vituo vyote vya kutolea huduma kuwa ni wazee wenye umri zaidi ya miaka 60,
watoto chini ya miaka mitano,watoto waishio katika mazingira hatarishi,
wajawazito na watu wasiojiweza kiuchumi.
Aliongeza kuwa
watu wengine ambao wapo kwenye makundi maalumu ni wenye magonjwa
sugu kama Kifua kikuu, Ukimwi, Kisukari, Magonjwa ya Moyo, Pumu,
Sikoseli, Ukoma, Saratani na Magonjwa ya Akili.
Aidha alisema kuwa
katika kuweka uwiano sawa kwa Watanzania wote bila ubaguzi Serikali
ya awamu ya tano ina pendekezo la kutoa bima ya afya ya lazima kwa watu wote
ambapo utasaidia pia kwa watu wenye msamaha kupata huduma bora.
Kama Serikali
itapitisha pendekezo la kutoa bima ya afya ya lazima kwa Watanzania wote
litasaidia upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment