Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Desemba, 2016
ameungana na wananchi wenzake Wilayani Chato mkoani Geita kutoa pole kutokana
na kifo cha Mzee Admirabilis Mbabe Manyama ambaye ni mzee maarufu wilayani hapa
na Mzee James Lufunga Mchele ambaye ni jirani yake.
Rais Magufuli pamoja na kuwapa pole wafiwa na
wananchi wa Chato kwa kuondokewa na mpendwa wao pia amitaka familia ya mzee
Manyama kuendelea kuishi kwa kushikamana na kupendana kama ilivyokuwa enzi za
uhai wa marehemu na kuwataka kuepukana na mifarakano.''Unapotokea msiba kama huu katika familia nyingi huzuka mifarakano, ombi langu kwenu wewe Mama mkubwa na Mama mdogo kamwe msikubali kufarakanishwa kutokana na kifo cha mume wenu,muwaongoze watoto wenu ili muendelee kuishi kwa kupendana kama enzi za uhai wa mzee''
Aidha Rais Magufuli amemuelezea Marehemu Mzee Manyama kuwa alikuwa mzee maarufu kijijini hapa na miongoni mwa mafundi hodari wa kushona nguo ambaye pia alimshonea sare zake za shule wakati akisoma.
Kwa upande wake Mdogo wa marehemu ambaye ni msemaji wa familia Bwana Deodatus Manyama ambaye ni msemaji wa familia amemshukuru Rais Magufuli pamoja na ujumbe wake alioambatana nao kuwapa pole katika msiba huo, na kwamba kitendo hicho kinaonyesha kuwa Rais magufuli si mtu asiejikweza wala asiye na majivuno.
Marehemu Mzee Admirabilis Mbabe Manyama amefariki akiwa na umri wa miaka 80,ameacha wajane wawili,watoto 15 na wajukuuu kadhaa.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato, Geita.
29 Desemba, 2016.
No comments:
Post a Comment