Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA)
imeunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kudhibiti upandashaji holela wa
nauli kwa mabasi yaendayo mikoani wakati wa kipindi hiki cha sikukuu za mwisho
wa mwaka.
Hayo yamesemwa jana na Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo David
Mziray wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hii, akieleza namna
mamlaka hiyo inavyodhibiti upandaji wa nauli za mabasi yaendayo mikoani.
“Kuna timu ambazo ziko katika vituo vyote vya mabasi makubwa
katika kila mkoa, timu hizo zinathibiti masuala ya nauli, usalama wa magari ,
kuhakikisha leseni za mabasi pamoja na muda uliopangiwa kuondoka vituoni,”
alifafanua Mziray.
Aliongeza kuwa mamlaka hiyo imeruhusu mabasi yanayobeba abiria
40 na kuendelea kuomba leseni za muda za kusafirisha abiria katika mikoa
ambayo ina wasafiri wengi zaidi katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.
Kwa mujibu wa Mziray alisema mabasi hayo yatakuwa yakikaguliwa
kwanza ndipo yanapewa leseni za muda pamoja na kupangiwa nauli ambazo watatozwa
abiria kutokana na mkoa ambao gari hilo litakwenda.
Akizungumzia kikosi kazi hicho, Mziray alisema kuwa mwanzoni mwa
wiki hii timu iliyoko kituo cha mabasi cha Ubungo ilikamata mabasi manne ambayo
yalipandisha nauli kwa abiria na kuchukuliwa hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment