Tuesday, 13 December 2016

KAHAMA OIL MILLS LIMITED YATOA AJIRA KWA WATU 600



Meneja Utawala na Uzalishaji wa Kampuni  ya Kahama Oil Mills Bw. Bryason Edward akipokea cheti cha ushiriki wa maonesho ya kwanza ya viwanda vya Tanzania kutoka kwa Katibu Mkuu waWizara ya Viwanda, Biashara na Uwezeshaji Dkt. Adelhelm Meru wakati wa hafla  ya kufunga maonesho hayo jana  jijini  Dar es Salaam.




Meneja Utawala na Uzalishaji wa Kampuni  ya Kahama Oil Mills Bw. Bryason Edward akishiriki hafla ya kufunga maonesho  ya kwanza  ya viwanda vya Tanzania yalio malizika katika viwanja vyaMwl. Nyerere (sabasaba) jana jijini Dar es Salaam.




Katibu Mkuu wa Wizara  ya Viwanda,  Biashara na Uwezeshaji Dkt. Adelhelm Meru akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja Utawala na Uzalishaji wa Kampuni ya Kahama Oil Mills Bw. Bryason Edward alipotembelea maonesho ya Viwanda vya Tanzania  jana Jijini Dar es Salaam . Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo  ya Biashara Tanzania (TANTARDE) Bw. Edwin  Rutageruka.
Kampuni ya Kahama Oil Mills iliyopo katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imeisaidia Serikali katika kupunguza tatizo la ajira kwa kuajiri jumla ya watu 639.

Idadi hiyo imetajwa jana Jijini Dar es Salaam na Meneja Uzalishaji wa kampuni hiyo, Bryason Edward alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii wakati wa kumalizika kwa Maonesho ya Kwanza ya Viwanda vya Tanzania yaliyofanyika katika viwanja vya Sabasaba vilivyopo jijini humo.

Edward amesema kuwa wameamua kushiriki katika maonesho hayo kwa ajili ya kubadilishana mawazo na wajasiriamali wengine pamoja na kuwaonyesha Watanzania bidhaa mbalimbali zilizokuwa zikizalishwa nje ya nchi ambazo kwa sasa zinazalishwa na kupatikana hapa hapa nchini.

 “Mpaka sasa kampuni yetu ina matawi 6 nchi nzima yaliyopo Kahama, Shinyanga, Mwanza, Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma ambayo ndio yamewezesha kuajiri jumla ya watu 639, hayo yote yametokana na kuona fursa na kuthubutu kuzitumia fursa hizo,”alisema  Edward.

Ameongeza kuwa ingawa kampuni hiyo bado changa lakini inajitahidi kutoa ajira hasa kwa vijana ili kuwasaidia katika kuendeleza maisha yao pamoja na kuwapatia mafunzo juu ya mambo mbalimbali yanayohusu ujasiriamali ili waweze kupata hamasa ya kuanzisha viwanda vyao vitakavyowasaidia kujiajiri.

Aidha, Edward ametoa rai kwa vijana kujishughulisha na kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo kwenye jamii zao ambazo zitawawezesha kujiajiri na kujipatia kipato kwa njia zilizo halali kuliko kujibweteka kusubiri kuajiriwa.

Ameiomba Serikali kurejea upya tozo za uingizaji wa vifaa kwa ajili ya utengenezaji wa mabati ili ziweze kupunguzwa hivyo kuwasaidia wajasiriamali kupata kipato kinacholingana na biashara hiyo.


Kampuni hiyo imeanzishwa mnamo mwaka 2005, inajihusisha na uchambuaji wa pamba na uzalishaji wa mafuta ya pamba pia inazalisha mabomba na vyombo vya plastiki pamoja na mabati ya aina zote.  

No comments:

Post a Comment