Waziri wa Katiba na
Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema serikali inatarajia kujadili kushusha
kiwango cha fedha kinachohusika katika makosa ya rushwa na uhujumu uchumi
kwenye mahakama ya mafisadi ili kukomesha vitendo vya rushwa.
Mwakyembe alitoa kauli
hiyo jana mara baada ya kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda.
“Nimeulizwa sana na waandishi wa habari tangu Julai hadi sasa
walitegemea kungekuwa na kesi nyingi lakini kuna kesi moja katika Mahakama ya
Mafisadi tumekuja kubaini kwamba uchache wa kesi ndiyo mafanikio makubwa ya
hatua ya kisheria tuliyochukua,”amesema.
Aliongeza kwa sasa
waliozoea kupora mabilioni wamerudi nyuma ambapo wezi hao wameonekana wakiiba
fedha chini ya Sh bilioni moja iliyopo kisheria hivyo wanategemea kujadili
sheria hiyo ili iwalenge hata wanaochukua kiasi kidogo.
“Sisi kama serikali tukiona wizi sasa umenza
kupungua na kuenea katika viwango vya Sh milioni 400, 500, 700 tumeanza
kujadiliana kuangalia uwezekano wa kushusha kiwango cha fedha ili tuweze
kukomesha kabisa udokozi, ubadhilifu, wizi wa fedha au mali ya umma,”alisema.
Aidha alifafanua
uamuzi wa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda kutafuta vijana wanaojua sheria ili
kusaidia wananchi kabla ya kwenda mahakamani ni mzuri.
Aliongeza kuwa tayari
wamepeleka mswada wa msaada wa kisheria ambao utasaidia wananchi hasa wa
vijijini na wanawake ambao ndiyo wanaumizwa na desturi zilizopitwa na muda ili
kuwasaidia kupata haki na itakuwa na wasaidizi wa kisheria nchi nzima wapatao
4,900.
Makonda alisema
wamejadili utoaji na upatikanaji wa haki kwa wakati kwani kuna changamoto ya
watu kuwa wengi na kuchelewa kupata haki zao.
Alisema kwa kuona adha
hiyo mkoa huo kwa kushirikiana na Wakuu wa wilaya watajenga Mahakama za Mwanzo
20 ili kuongeza kasi za utoaji na upatikanaji wa haki kwa wananchi endapo
wanapopelekwa vituo vya polisi.
No comments:
Post a Comment