Serikali imesimamisha
shughuli za Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la Korosho ili kupisha uchunguzi
wa matumizi ya fedha za mfuko huo.
Hatua hiyo
imechukuliwa baada ya Mfuko huo kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu
pamoja na kuwepo kwa malalamiko ya muda mrefu kuhusu utendaji wa mfuko huo.
Uamuzi huo
umechukuliwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt.
Charles Tizeba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio na
changamoto ya zao hilo.
Dkt. Tizeba alisema
kuwa lengo la uanzishwaji wa mfuko huo lililoafikiwa na Serikali pamoja na
wadau wa korosho limekuwa halifanani na utekelezaji wake kwani maendeleo yote
yanayoonekana kwenye zao hilo hayatokani na uwepo wa mfuko bali yanatokana na
nguvu ya Serikali.
“Baada ya kutafakari
utendaji wa mfuko huo tumegundua kuwa mfuko umeshindwa kutimiza malengo
yaliyodhamiriwa, umeshindwa kusimamia na kutekeleza maelekezo mbalimbali
yanayotolewa na Bodi ya Korosho hivyo tumeamua kusitisha shughuli za mfuko huo
na kuanzia leo shughuli hizo zitatekelezwa na Bodi ya Korosho mpaka hapo
tutakapotoa maelekezo mengine.”alisema Waziri huyo.
Waziri aliongeza
sababu nyingine za kusitishwa kwa Mfuko huo ni kujihusisha na vitendo
vinavyohujumu wakulima wa zao hilo hasa wakati wa ununuzi wa pembejeo pamoja na
kununua viuatilifu vilivyo chini ya kiwango kwa bei kubwa, matumizi mabaya ya
fedha kinyume cha Sheria na Kanuni za mfuko pamoja na kushindwa kutekeleza
agizo la Serikali kwa kuweka fedha kwenye amana za muda maalumu katika Benki
mbalimbali badala ya kupeleka Benki Kuu.
Aidha, Dkt. Tizeba
alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania anapowasilisha fedha
zilizokusanywa na watu wanaosafirisha korosho nje ya nchi kuwasiliana kwanza na
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho ili kufahamu usimamizi na utaratibu wa fedha
hizo.
Kwa upande mwingine,
Dkt. Tizeba ameizuia Menejimenti ya mfuko huo kufanya muamala wowote wa fedha
za mfuko mpaka hapo maelekezo ya hatima yao yatakapotolewa na badala yake
miamala yote itafanyika kwa utaratibu utakaopangwa na Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Ameiagiza Bodi ya
Korosho kusimamia kwa haraka jukumu la upatikanaji wa pembejeo na viuatilifu
kwa sababu msimu wa zao hilo umekaribia.
No comments:
Post a Comment