Friday 23 February 2018

MAKAMU WA RAIS AITAKA SIMIYU KUENDELEZA MPANGO WA EQUIP-TANZANIA




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongea na wadau wa Elimu Mkoani Simiyu, leo wakati wa Kongamano kubwa la Elimu ya Juu lililoandaliwa na Chuo Kikuu Huria Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.





Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akimuelezea Makamu wa Rais (hayupo pichani)  namna utekelezaji wa mpango wa EQUIP-Tanzania unavyofanyika mkoani humo katika kongamano la Elimu ya Juu lililofanyika leo, mkoani humo.





Mkuu wa DFID-Tanzania Bibi Elizabeth Arthy akizungumza mbele ya Makamu wa Rais juu ya mchango wa Serikali ya Uingereza katika kuboresha elimu nchini Tanzania katika kongamano la Elimu ya Juu lililofanyika leo, mkoani Simiyu.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaagiza watalaamu wa elimu na viongozi wa Mkoa wa Simiyu kuhakikisha wanaendeleza Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (EQUIP-Tanzania) unaotekelezwa na Serikali kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la nchini Uingereza (DFID).

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo leo Mkoani Simiyu alipokuwa akiongea na viongozi na watumishi wa Serikali wa Mkoa huo  katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku tano mkoani humo.

"Mpango huu umekuwa na mafanikio makubwa kwa Mkoa wa Simiyu, kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa ya darasa la Saba ambapo Mkoa umetoka kushika nafasi za mwisho Kitaifa hadi kufikia nafasi ya 11 mwaka 2017.

Amesema mafanikio ya mpango huo yamekuwa makubwa, huku akishukuru shirika la DFID kwa mchango wao mkubwa ikiwa ni pamoja na kutoa kiasi cha fedha shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule.


Aidha, Mhe. Samia ameutaka uongozi wa mkoa huo kuhakikisha Mpango huo unaendelezwa hata baada ya wafadhili hao kumaliza muda wao ili kuhakikisha kiwango cha elimu kinaendelea kuboreka kila mwaka.
Mhe. Samia amemuhakikishia Kiongozi Mkuu DFID-Tanzania Bibi Elizabert Arthy kuwa nchi ya Uingereza itaendelea kufanya kazi na Serikali katika kuboresha elimu nchini.

Kwa upande wake, Elizabeth Arthy amesema katika kuhakikisha wanapambana na hali ya kuboresha elimu nchini tayari Mkoa wa Simiyu umepewa fedha kutoka DFID kiasi cha shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka ameishukuru DFID kwa ufadhili wake kupitia EQUIP-Tanzania ambapo ufaulu wa wanafunzi umeongezeka mkoani humo  kutoka asilimia 36 mwaka 2013 mpaka 68 mwaka 2017.


Katika kipindi cha miaka Minne DFID imewekeza katika mpango wa kuinua ubora wa elimu mkoani Simiyu kwa kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 9.

No comments:

Post a Comment