Monday 26 September 2016

ALIYOAGIZA LEO RAIS MAGUFULI BAADA YA KUFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA BANDARINI JIJINI DSM

Leo September 26 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametembelea Bandari ya Dar es Salaam na kuzungumza na wafanyakazi wa bandari hiyo ambapo pamoja na mambo mengine ametoa miezi miwili kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kununua mashine nne za kukagulia mizigo bandarini (Scanning Mashine).

Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kubaini kuwa kati ya mashine nne za ukaguzi wa mizigo zilizopo, ni mashine mbili tu ndizo zinafanya kazi na hazina uwezo wa kukagua mizigo yote inayotoka na kuingia nchini kupitia bandari hiyo hali inayosababisha kutokuwepo kwa udhibiti wa uhakika wa udanganyifu.

“Kwa hiyo nawaagiza TPA, na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Mbarawa na Mamlaka ya Mapato mpo hapa hakikisheni mnanunua mashine za kukagulia mizigo nne ndani ya miezi miwili, na ikifika miezi mitano
 muwe mmenunua mashine sita, ni lazima mizigo yote ikaguliwe kwa mashine” 

Dkt. Magufuli ameiagiza (TPA) kwa kushirikiana na Wizara husika kuanza mazungumzo na kampuni ya kimataifa ya kuhudumia shehena ya makasha bandarini (TICTS) ambayo inapakia na kupakua mizigo katika gati namba nane hadi kumi na moja ili kurekebisha mkataba ambao Kampuni hiyo imeingia na Serikali kwa lengo la kuhakikisha nchi inapata manufaa yanayostahili.

Rais Magufuli alitetembelea eneo la mita za kupimia mafuta yanayopakuliwa melini (Flow Meters) na kubaini kuwa mita hizo hazifanyi kazi, ameiagiza TPA kuharakisha mchakato wa kununua mita mpya na kuzifunga katika eneo hilo ili kudhibiti ukusanyaji wa mapato ya kodi ya mafuta. 
Aidha, Dkt. Magufuli ameitaka TPA kujipanga kujenga bandari kavu (ICD) katika eneo la Ruvu Mkoani Pwani ili kuachana na bandari kavu zilizoanzishwa na watu binafsi hapa Jijini Dar es Salaam na ambazo zimekuwa zikitumika kukwepa kodi.

No comments:

Post a Comment