Monday 4 July 2016

YANGA NA MEDEAMA KUCHEZA JUMAMOSI YA JULAI 16 TAIFA


Mawinga wa Yanga, Simon Msuva (kulia) na Geoffrey Mwashiuya (kushoto) wakiwa mazoezini leo Uwanja wa Boko Veterani

MECHI ya Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika kati ya wenyeji, Yanga SC na Medeama ya Ghana itachezwa Jumamosi ya Julai 16, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro leo mjini Dar es Salaam.

Muro amesema tayari wamekwishatuma taarifa za muda na siku ya kuchezwa mechi hiyo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na hawana shaka mambo yatakuwa kama yalivyopangwa.

Yanga imejitahidi safari hii kuitaarifu mapema CAF juu ya siku na muda wanaotaka kucheza mechi yao, baada ya kujikuta wakicheza mechi iliyopita dhidi ya TP Mazembe kinyume na matakwa yao.
Yanga ilifungwa 1-0 na Mazembe ya DRC Jumanne ya Juni 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo waliotaka wacheze Jumatano usiku.
Hata hivyo, CAF iliwakatalia Yanga kuupeleka mbele mchezo huo kwa kuwa walichelewa kutuma taarifa za mabadiliko – na mechi dhidi ya Mazembe kama wasingetoa taarifa mapema ingechezwa Jumapili ya Julai 17.    
Yanga itakuwa inasaka ushindi wa kwanza katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Julai 16, baada ya kupoteza mechi zote mbili za kwanza, mbali na Mazembe, pia walifungwa 1-0 na MO Bejaia nchini Algeria Juni 19, mwaka huu.
Baada ya Raundi mbili za mwanzo, TP Mazembe inaongoza Kundi A kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na Bejaia pointi nne, Medeama pointi moja wakati Yanga inashika mki ikiwa haina pointi.


No comments:

Post a Comment