Wednesday 13 July 2016

MIFUPA YA BINADAMU YADAIWA KUONEKANA KANDO YA ZIWA VICTORIA


Hali ya sintofahamu juzi Imewakumba wakazi wa Kijiji cha Ihumilo Kata ya Nkome wilaya na Mkoa wa Geita baada ya mifupa ya binadamu anayedaiwa kuzikwa zaidi ya miaka 10 iliyopita kuonekana kandokando ya Ziwa Victoria.
Mifupa hiyo iliyoonekana ikiwa imehifadhiwa kwenye kipande cha karatasi ya plasitiki nyeusi ilionekana tangu Julai 7 mwaka,katika mwalo wa Mchangani baada ya kaburi lake kufukuliwa na mawimbi ya maji kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji ya Ziwa Victoria.

Mwenyekiti wa Kitongoji Cha Mchangani Simoni  Malole amesema mifupa hiyo ni ya mtu aliyezikwa kati ya mwaka 2006 na 2007,baada ya kufa maji na mwili wake kuonekana ukielea juu ya maji na alizikwa eneo hilo kwa kukosa ndugu.

Mifupa hiyo iliondolewa juzi na wananchi na kwenda kuzikwa eneo jingine baada ya mahakama ya Nyamboge Kutoa kibali kwa mujibu wa sheria na zoezi hilo kusimamiwa na askari polisi wa kituo kidogo cha Nkome chini ya Mkuu wake Inspekta Ndege.


Aidha Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ihumilo John  Misango amewataka wananchi kuacha taboa ya kuzika kandokando ya ziwa na badala yake wanapaswa kutunza mazingira ya ziwa kwa mujibu wa sheria.

No comments:

Post a Comment