Wednesday 6 July 2016

SIMBA WAENDA MOROGORO KUWEKA KAMBI, WAKIRUDI WANAKIPIGA NA GOR MAHIA



SIMBA SC inatarajiwa kuondoka mjini Dar es Salaam keshokutwa kwenda Morogoro kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambao utanatarajiwa kuanza kuanzia Agosti 20, mwaka huu.

Na baada ya maandalizi mazuri ya takriban mwezi mzima, Simba imeialika klabu bingwa ya Kenya, Gor Mahia kwa ajili ya kuja nchini kucheza mechi ya kirafiki katika Tamasha la Simba Day, Agosti 8.
 Rais wa Simba, Evans Elieza Aveva alisema kwamba uongozi wa timu hiyo uliamua kuahirisha programu ya mazoezi iliyopangwa kuanza jana mjini Dar es Salaam kwa ajili ya kupisha sherehe za Sikukuu ya Eid El Fitri.
Rais wa Simba, Evans Aveva akimkabidhi jezi kocha Omog wiki iliyopita baada ya kusaini Mkataba wa miaka miwili
Meneja huyo wa zamani wa Embassy Hotel, Aveva alisema kuwa wachezaji wote waliosajiliwa na timu hiyo watakwenda kambini Morogoro kwa ajili ya kuanza kujifua wakiwa chini ya Kocha Mkuu mpya Mcameroon Joseph Marius Omog ambaye aliwasili nchini wiki iliyopita na kurithi mikoba ya Muingereza Dylan Kerr, aliyefukuzwa Januari.

"Kila kitu kinakwenda vizuri na Mungu akijaalia baada ya sikukuu kupita, timu itakwenda Morogoro na si Lushoto kama ilivyoandikwa na gazeti moja," alisema Aveva.


No comments:

Post a Comment