Thursday 12 January 2017

MIAKA 53 YA MAPINDUZI MATUKUFU YA ZANZIBAR YAPIGA HATUA ZA KIMAENDELEO



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein akikagua gwaride katika sherehe za miaka 53 ya mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika katika uwanja wa Amani, Zanzibar.



Vijana vya halaiki wakiwa katika umbo linaloonesha miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar katika sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Amani, Zanzibar.



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein akiongea na wananchi wakati wa sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambapo alisema mbali na jitihada zilizofanywa na serikali hiyo katika kuinua maisha ya Wazanzibar ameahidi kuendelea kusimamia rasilimali ili zitumike kwa maslahi ya wananchi wote.
Zanzibar imeadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu huku ikiwa imepiga hatua mbalimbali za kimaendeleo na utoaji wa huduma bora za kijamii.

Hayo yamebainishwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein wakati akihutubia wananchi katika sherehe za maadhimisho ya Mapinduzi leo katika uwanja wa Amani, Unguja, Zanzibar.

Dkt. Sein amesema kuwa siku ya Mapinduzi ni muhimu sana katika historia ya Zanzibar kwani ndiyo siku ambayo Wazanzibar walipokuwa huru katika nchi yao na kuweza kufanya shughuli mbalimbali za kujiletea maaendeleo.

“Tukiwa tunasherehekea miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ni vyema tukajivunia maendeleo yaliyopatikana na yanayoendelea kupatikana.”Alisema Dkt. Shein.

Akitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana tangu Mapinduzi Matukufu yatokee tarehe 12 Januari 1961, Dkt. Shein amesema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta za elimu kwa kuwa na ongezeko la shule kutoka shule 752 mwaka 2015 hadi kufikia 843 mwaka 2016.

Ongezeko hilo limeenda sambamba na ongezeko la udahili wa wananfunzi ambapo umeongezeka kutoka wanafunzi 384,000 hadi kufikia 424,000 mwaka 2016.

Katika sekta ya afya kumekuwa na mafanikio ya kuongezeka kwa vituo vya afya kwa asilimia 13.4 ambapo mwaka 2015 kulikuwa na Vituo vya Afya 134 hadi kufikia sasa jumla ya Vituo 152 vimepatikana.

Mafanikio mengine ni pamoja na upatikanaji wa ajira 2658 zilizotokana na miradi mbalimbali iliyozindulia katika kipindi hiki cha maadhimisho ya siku ya Mapinduzi, kukua kwa Sekta ya Utalii kwa ongezeko la watalii kwa asilimia 13 huku ikichangia pato la taifa kwa asilimia 27.

Huduma za kijamii zimezidi kuboreshwa huku upatikanaji wa maji safi na salama umeendelea kutatuliwa ambapo miradi ya maji imeekuwa ikitekelezwa ikiwemo kuchimba visima vipya 9 na kuvifanyia ukarabati visima vya zamani.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd amesema kuwa Mapinduzi haya yamekuwa chachu ya kuleta maendeleo kwa kuwa yamewaweka Wazanzibar kuwa huru katika kutekeleza shughuli zao za kujiletea maendeleo.

Zanzibar imeadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar huku ikiwa imepiga hatua kubwa za kimaendeleo ambapo katika shamra shamra za maadhimisho haya jumla ya miradi 32 ya maendeleo imezinduliwa huku mingine 16 ikiwekwa jiwe la msingi tayari kwa utekelezaji wake, hayo yote ni matunda yatokanayo na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo baadaye yalizaa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.



No comments:

Post a Comment