Thursday 26 January 2017

RAIS MAGUFULI KUWA MGENI RASMI SIKU YA SHERIA NCHINI



Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma akiongea na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kitakachofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Mahakama vilivyopo jijini Dar es Salaam.


Jaji Kiongozi wa Mahakam Kuu Tanzania Jaji Ferdinandi Wambali (kushoto) akiongea na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kitakachofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Mahakama vilivyopo jijini Dar es Salaam.


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Katrina Revocati akiongea na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kitakachofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Mahakama vilivyopo jijini Dar es Salaam.
Rais John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Sheria nchini zitakazofanyika mwanzoni mwa mwezi ujao katika viwanja vya Mahakama jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam Kaimu Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema mahakama itawaelimisha wananchi jitihada mbalimbali ilizochukua zenye lengo la kuboresha huduma zake kupitia mpango mkakati wa miaka mitano inaoutekeleza katika kutoa haki kwa wakati na kuwezesha ukuaji wa uchumi.

Amesema kabla ya kilele cha maadhimisho hayo, mahakama itafanya matembezi maalum yatakayoongozwa na Rais Mstaafu Mh. Ali Hassan Mwinyi  na yataanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuishia katika viwanja vya Mnazi mmoja

Katika matembezi hayo Mhe. Rais Mstaafu Mwinyi atazindua rasmi maadhimisho ya wiki ya elimu ya sheria ikiwa ni sehemu ya sherehe za kuelekea maadhimisho ya kilele cha siku ya sheria nchini.
Aidha ametoa rai kwa wananchi kutembelea sehemu zote zilizoandaliwa kwa ajili ya utoaji elimu ya sheria nchini kwa ajili ya kujifunza na kupata huduma mbalimbali za Kisheria

Alizitaja huduma hizo ni pamoja na taratibu za ufunguaji mashauri katika ngazi mbalimbali za mahakama, taratibu za kesi za mirathi, taratibu za kesi za dhamana, taratibu za rufaa, ndoa na talaka, taratibu za kupokea na kushughulikia malalamiko na Msaada wa Kisheria

Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini hufanyika kila mwaka mwanzoni mwa mwezi wa pili na mwaka huu yamebeba ujumbe wa Umuhimu wa Utoaji Haki kwa Wakati Kuwezesha Ukuaji wa Uchumi.

No comments:

Post a Comment