Thursday 19 January 2017

SERIKALI KUWAPATIA VIJANA STADI ZA KAZI ILI WASHIRIKI KWENYE UCHUMI WA VIWANDA

 

Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) Prof.Preksedis Ndomba (kushoto) na Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bw. Ally Msaki wakisaini makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi hiyo utakaowezesha vijana kupata mafunzo ya uzalishaji wa mazao ya ngozi katika Taasisi hiyo Kampasi ya Mwanza ili kuchochea uchumi wa viwanda nchini.
Serikali imepanga kutumia bilioni 15 kuwapatia vijana stadi za kazi zitakazowawezesha kujiajiri na kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam wakati wa kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano kati ya Taasisi ya Teknolojia Dar es saalam (DIT) na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Akizungumzia makubaliano hayo Mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Ally Msaki amesema kuwa yatasaidia kuiwezesha Taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa vijana hasa ya kuzalisha bidhaa zitokanazo na ngozi ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

“Vijana 1000 wataanza kupata mafunzo mwezi Februari mwaka huu na yatakayohusu utengenezaji wa bidhaa za ngozi na program hii ipo ndani ya mpango wa miaka mitano.” Alisema Msaki.
Mafunzo hayo ya stadi za kazi kwa vijana yatagharimiwa na Serikali na yatahusisha vijana walio katika mfumo rasmi na wale wasio katika mfumo rasmi wa elimu lengo likiwa ni kuwakwamua vijana ili washiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.

Akifafanua Msaki alisema kuwa dhamira ya Serikali ni kuwawezesha vijana baada ya mafunzo hayo kujiajiri na kuwaajiri wenzao hivyo kuondokana na tatizo la ajira na kuongeza nguvukazi ya taifa kwenye uzalishaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) Prof.Preksedis Ndomba alibainisha kuwa Taasisi hiyo imejipanga vyema kuwawezesha vijana kwa kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya soko na kuweka msisitizo katika mafunzo kwa vitendo.

Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) ipo imedhamiria kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kufikia uchumi wa kati.

No comments:

Post a Comment