Saturday 21 January 2017

SERIKALI KUPITIA UPYA KANUNI ZA UTANGAZAJI



Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye 
Serikali imejipanga kupitia upya kanuni za utangazaji za Sheria ya Utangazaji ya mwaka 2003 ili kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye wakati wa ziara yake kwa vyombo vya habari vya Channel, na Tumain Media iliyolenga kuimarisha mahusiano yaliyopo kati ya Serikali na vyombo vya habari nchini.

Waziri Nape amesema kuwa lengo la mapitio ya kanuni hizo ni uboreshwaji wa kanuni hizo ili kuisaidia kukuza sekta ya utangazaji.

“Kuna baadhi ya wadau wamekuwa wakilalamika kuhusu kupitwa kwa wakati kwa kanuni hizo, hivyo tumeona ni vyema kuungana nao ili kuzipitia upya na kuona palipo na mapungufu” alisema Waziri Nape.

Aidha, Waziri Nape aliongeza kuwa baadhi ya maeneo katika kanuni hizo yanayohitaji kupitiwa upya ni aina za leseni zilizopo, kubadilika kwa jamii inayotuzunguka pamoja na mabadiliko ya teknolojia yanayokuwa kwa kasi.

Mbali na hayo Waziri Nape amesema kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) ipo katika hatua za mwisho za kuandaa kanuni za kudhibiti masuala ya matumizi ya mitandao ya kijamii nchini.

Katika hatua hiyo Waziri Nape amewataka wadau mbalimbali kutoa maoni ili kusaidia kuboresha kanuni za mitandao ya kijamii kwa lengo ili kukuza tasnia ya habari. 

Hata hivyo, Waziri Nape ameahidi kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari nchini katika kutoa habari kwa ajili ya kuhabarisha umma kuhusiana na mambo mbalimbali yahusuyo Serikali katika kutekeleza majukumu yake.

“Kwa yeyote atakayepata changamoto ya aina yeyote kutoka kwa watumishi wa Serikali ikiwemo ya upatikanaji wa habari milango ipo wazi katika kurepoti changamoto hiyo” alisisitiza Waziri Nape.

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye yupo katika ziara ya kutembelea vituo vya Televisheni kujionea utendaji kazi wa vituo hivyo ikiwa pamoja na changamoto zilizopo ili kupata namna bora ya kuiendeleza sekta ya habari kwa manufaa ya taifa, mpaka sasa ameshatembelea Kampuni nane za vyombo vya habari.



No comments:

Post a Comment