Spika wa Bunge,
Mhe. Job Ndugai amefunguka na kusema atakwenda jijini Nairobi nchini
Kenya kumuona Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye anafanyiwa
matibabu katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya kufuatia kupigwa risasi
Septemba 7, 2017.
Job Ndugai amesema
hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma nyumbani
kwake na kusema kuwa watakwenda kumuona Tundu Lissu kwani ni mbunge wao na wao
wanampenda sana na kudai kuwa kipindi cha nyuma alishindwa kwenda Kenya kwa
kuwa nchi hiyo ilikuwa kwenye uchaguzi na haikuwa na utulivu wa kisiasa ila kwa
kuwa saizi imetulia anatarajia kwenda baada ya Christmas kumjulia hali.
"Mimi kama Spika
siwezi kwenda na kutoka navyotaka Kenya bali napokwenda kule lazima kuwe na
taarifa rasmi za kiserikali na kibunge na ninapokelewa hivyo na ninapopelekwa
huko hospitali au wapi napelekwa kwa utaratibu huo ndiyo utaratibu wa nchi kwa
nchi. Haiwezekani wao wana mechi kama zile (Uchaguzi) halafu spika nazunguka
zunguka Nairobi wanaweza kusema ajenda aliyokuja nayo huyu siyo hii, katika
pande hizi mbili Watanzania wamemtuma huyu ana ajenda nyingine kwa hiyo
unapokuwa kiongozi lazima ujiongeze" alisema Spika Ndugai
Ndugai aliendelea
kueleza kuwa "Haukuwa wakati mzuri kwenda Nairobi, ila kwa kuwa haya mambo
yamepita na serikali saizi imekaa sawa sawa basi tusubiri Christmas ipite baada
ya hapo mtamuona Spika muda si mrefu akienda kumuona Mbunge wake Nairobi au
mahali pengine popote pale, yule ni Mbunge wetu na tunampenda sana na
tusingependa asikitike kwa lolote lile" alimalizia Ndugai
Mbunge Tundu Lissu
alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 akiwa mjini Dodoma na baadaye
kupelekwa nchini Kenya jijini Nairobi kwa matibabu ambapo mpaka sasa yupo huko
anaendelea na matibabu.
No comments:
Post a Comment