Jeshi la polisi mkoani
Mwanza linamshikilia mtu mmoja kwa kosa la kujifanya daktari, katika hospitali
ya mkoa Sekou Toure.
Joseph Mbagata
25,mkazi wa mtaa wa Mabatini jijini humo amekamatwa leo Desemba 18 na
jeshi hilo baada ya kubainika kwamba sio mwanataaluma na alikuwa akiwatapeli
wagonjwa kwa kuwaomba hongo, kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Taarifa kutoka kwa
jeshi hilo zimesema kwamba mtuhumiwa alikuwa akiwaomba hongo, huku akiahidi
kuleta dawa muhimu na pia kufanya mipango ili mgonjwa apate huduma kwa haraka.
Awali zilipatikana
taarifa kuwa siku chache zilizopita alionekana mtu aliyevalia mavazi ya
udaktari na kujifanya daktari, kisha anapita wodini kuwaona wagonjwa. Pia
ilisemekana kuwa mtu huyo tayari amechukua Sh30,000 kwa mgonjwa ili aweze
kumpatia matibabu.
Aidha baada ya tuhuma
hizo kufika katika uongozi wa hospitali waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata
mtuhumiwa, akiwa amevalia mavazi ya udaktari huku akiwa amesimama nje ya wodi
ya upasuaji.
“Tumekuwa
tukilalamikiwa kwamba kuna baadhi ya madaktari hapa hawana ujuzi wala
hawajitambui, kumbe ni dhahiri kwamba hao watu wapo na kuanzia sasa lazima
tufanye ukaguzi wa hali ya juu ili hali hiyo isije ikajitokeza tena maana ni
sehemu ya kuhatarisha maisha,” amesema mmoja wa madakatri katika
hospitali hiyo ambaye hakutaka kutajwa majina.
Baada ya daktari huyo
feki kukamatwa, uongozi wa hospitali ulitoa taarifa polisi, ambapo askari
walifika eneo la tukio na kumuweka mtuhumiwa chini ya ulinzi kisha kumfanyia
upekuzi kwenye begi alilobeba na kukuta mavazi yanayotumiwa na madaktari katika
vyumba vya upasuaji.
Polisi wapo katika
upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa
atafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi
yake.
Kamanda wa polisi mkoa
wa Mwanza naibu kamishina wa polisi Ahmed Msangi ametoa wito kwa wananchi
hususani wagonjwa waliopo hospitalini akiwaomba kuwa makini na watu ambao ni
matapeli wa aina kama hiyo wenye nia ovu dhidi yao.
Aidha pia aliwaomba
viongozi wa hospitali zote kuendelea kutoa taarifa kwa polisi kuhusiana na watu
wanao watilia shaka hospitalini, ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika
vyombo vya sheria.
No comments:
Post a Comment