Jeshi la Polisi nchini
limetamba kushinda vita dhidi ya uhalifu baada ya kupunguza matukio ya aina
hiyo huku likikiri kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji na kunajisi.
Wakati hali ikiwa
hivyo, jeshi hilo limetoa tahadhari kwa watu ambao hujihusisha na uhalifu hasa
katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka kwa lengo la kutaka kujipatia
kipato kwa njia zisizo halali kuwa watachukuliwa hatua kali kwa kuwa
limejipanga kupambana nao.
Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz, alisema hayo jijini Dar es
Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hali ya usalama
nchini.
Alisema hali ya
usalama wa nchi kwa ujumla ni ya kuridhisha na kwamba takwimu zinaonyesha kuwa
kuanzia Januari hadi Novemba, mwaka jana, makosa makubwa ya jinai yalikuwa
68,204 ikilinganishwa na makosa 61,794 yaliyoripotiwa mwaka huu.
Hali hiyo imesababisha
upungufu wa makosa 6,410 ambayo ni sawa na asilimia 9.4.
Ubakaji Waongezeka
Hata hivyo, Kamishna
Boaz alisema makosa ya ubakaji na kunajisi yanaonekana kuongezeka kwa kuwa kwa
mwaka 2016 hadi kufikia Novemba, yaliyoripotiwa yalikuwa 6,935 kulinganisha na
makosa 7,460 ambayo yaliripotiwa mwaka huu.
“Hili ni ongezeko la
makosa 478 sawa na asilimia 6.8 wakati makosa ya kunajisi yalikuwa 16 mwaka
2016 ikilinganishwa na makosa 25 ambayo yametokea mwaka huu na kufanya ongezeko
la makosa tisa sawa na asililimia 56.3,” alisema.
Alisema kuna sababu
tatu ambazo zimechangia kuongezeka kwa matukio hayo ikiwamo mmomonyoko wa
maadili kwa kuwa kuna watu wanaparamia watoto wadogo. Pia alisema hali hiyo
inachangiwa na ushirikina kutokana na baadhi ya watu kuambiwa kuwa wakitembea
na watoto wadogo wanaweza kufanikiwa katika mambo fulani, lakini wakati
mwingine hiyo inatokana na tamaa za mwili.
“Sasa sababu hizo ni
kwamba tiba yake ipo kwenye jamii na sisi tutaweka msisitizo sana mwakani na
pengine mwisho wa mwaka kuhusiana na matukio hayo,” alisema Boaz.
Makosa dhidi ya Binadamu
Alisema makosa dhidi
ya binadamu ambayo yanajumuisha mauaji, kubaka, kulawiti wizi wa watoto, kutupa
watoto, kunajisi na kusafirisha binadamu yaliyoripotiwa katika kipindi cha
Januari hadi Novemba, 2016 yalikuwa 11,513 kulinganisha na 11,620 yaliyoripotiwa
mwaka jana ambayo ni ongezeko la makosa 107 sawa na asilimia 0.9.
Pia alisema makosa ya
wizi wa silaha, unyang’anyi katika barabara kuu, unyang’anyi wa kutumia silaha,
unyang’anyi wa kutumia nguvu, uvunjaji, wizi, wizi wa pikipiki, wizi wa magari,
mifugo pamoja na kuchoma nyumba moto mwaka jana yaliripotiwa 34,830 wakati
mwaka huu yameripotiwa makosa 29,677 ambayo ni pungufu kwa makosa 5,153 sawa na
asilimia 14.8.
Makosa ya uhalifu wa
kifedha
Boaz alisema makosa ya
noti bandia , wizi katika mabenki, wizi katika mashirika ya umma, wizi katika
vyama vya ushirika na makosa ya kughushi jumla ya yaliripotiwa makosa 1,861 kwa
mwaka jana ukilinganisha na mwaka huu yaliripotiwa makosa 1,526 ikiwa ni
pungufu ya makosa 335 sawa na asilimia 18.0.
Kwa upande wa uhalifu
katika jamii, alisema makosa hayo ni yale ambayo yanahusisha kupatikana na
silaha, dawa za kulevya, bangi, mashamba ya bangi, mirungi, nyaraka za
serikali, magendo, rushwa, uvuvi haramu, kupatikana na mazao ya bahari na
wahamiaji haramu.
Alisema makosa ya aina
hiyo yaliyoripotiwa kwa kipindi cha Januari hadi Novemba, mwaka huu yalikuwa
20,000 kulinganisha na makosa 18,971 yaliyoripotiwa mwaka jana.
Makosa ya Barabarani
Kuhusu makosa ya
usalama barabarani, alisema mwaka jana kuanzia Januari hadi Desemba
yaliripotiwa matukio 9,550 ikilinganishwa na 5,537 yaliyoripotiwa katika
kipindi kama hicho mwaka huu ikiwa pungufu ya matukio 4,013 sawa na asilimia
42.
Boaz alisema ajali
hizo zilisababisha vifo vya watu 3,108 na majeruhi 8,898 kwa mwaka 2016 wakati
mwaka huu watu waliokufa ni 2,491 na majeruhi 5,696.
“Uchunguzi umebaini
kuwa kiasi kikubwa, ajali zinasababishwa na vyanzo vikuu vitatu ambavyo ni
sababu za kibinadamu, ubovu wa vyombo vya usafiri na sababu za kimazingira.
“Sababu za kibinadamu
ni pamoja na uendeshaji wa hatari, uzembe wa madereva, uzembe wa abiria,
mwendokasi, uzembe wa watembea kwa miguu, ulevi, mifugo isiyochungwa na uzembe
wa waendesha pikipiki,” alisema.
Aidha, alisema katika
msimu wa sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, wamejipanga vyema kudhibiti vitendo
vyote vya uhalifu vitakavyojitokeza kwa kuwa ulinzi utaimarishwa katika maeneo
yote ikiwamo kwenye nyumba za ibada, fukwe za bahari, sehemu za starehe na
mengine ya mikusanyiko mikubwa ya watu.
No comments:
Post a Comment