Tuesday, 5 December 2017

MGODI WA DHAHABU WA GGM MABINGWA MICHEZO YA SHIMMUTA



Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM) umeibuka kidedea kwenye Mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Makampuni binafsi Tanzania (SHIMMUTA) yaliyomalizika Disemba Mosi kwenye Viwanja vya Samora Mjini Iringa
Katika mashindano hayo, Mgodi wa Dhahabu Geita umeibuka washindi wa Jumla kwenye Mpira wa Miguu Wanaume, Volleyball wanawake pamoja na Riadha wanaume Mita 100 na Riadha wanaume Mita 200. Vilevile, GGM imeshika nafasi ya pili katika Riadha wanawake Mita 200 na mchezo wa Basketball wanaume. Kampuni hiyo imekuwa mshindi wa Tatu kwenye Riadha wanawake Mita 400 pamoja na Mita 800.
Kwa Ushindi huo, Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM) umeibuka kidedea kwa kuwa mshindi wa jumla wa mashindano (overall winner) ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Makampuni binafsi Tanzania (SHIMMUTA).
Akizungumzia ushindi huo, Meneja Mawasiliano na Mahusiano  wa Mgodi wa Dhahabu Geita Bw Tenga B Tenga amesema kuwa ushindi huo ni uthibitisho kuwa Mgodi wa Dhahabu Geita unathamini michezo na kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya Tano kuinua michezo Tanzania.
“Mashindano ya Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma na Makampuni binafsi Tanzania ni michezo muhimu inayoimarisha uhusiano baina ya wafanyakazi kutoka Taasisi mbalimbali. Kampuni ya Geita Gold Mine imekuwa ikishiriki kila mwaka kwenye michezo hii ili kujenga afya bora kwa wafanyakazi wake na kujenga ujirani mwema kati ya Kampuni hiyo na Mashirika ya Umma na Makampuni binafsi Tanzania” alisema Bw Tenga.
Bw Tenga aliongeza kuwa Kampuni yake itaendelea kushiriki mashindano hayo ili kumuunga mkono mlezi wa Kitaifa wa Mashindano hayo Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samiah Suluh Hassan.

Mashindano hayo yanayosimamiwa na Mlezi wake ambae ni Makamu wa Raisi wa Jamuhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hasan, yalizinduliwa rasmi tarehe 22 November na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe  na Kombe la ushindi lilikabidhiwa kwa timu ya GGM na Mkuu wa mkoa wa Iringa Mheshimiwa Amina Masenza tarehe 1 disemba baada na kufunga mashindano hayo kwa mwaka huu.

No comments:

Post a Comment