Washtakiwa wanne
katika shauri la kufanya vitendo vinavyoashiria mapenzi ya jinsia moja na
makosa la kimtandao wameachiwa kwa dhamana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mwanza kutupilia mbali hoja za kuzuia dhamana zao zilizowasilishwa na upande wa
Jamhuri.
Uamuzi huo umetolewa
na Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Wilbert Chuma leo Desemba 15, baada ya
kukubaliana na hoja za mawakili wa utetezi, Mashaka Tuguta, Ogastini Kulwa na
Jebra Kambole kuwa hoja zilizowasilishwa na upande wa mashtaka ni dhaifu mbele
ya macho ya sheria.
Washtakiwa katika
shauri hilo namba 548/2017 ni Milembe Suleiman na Janeth Shonza wanaodaiwa
kuvishana pete ya uchumba licha ya wote kuwa wanawake.
Wengine ni Aneth Mkuki
anadaiwa kufanikisha sherehe wawili hao kuvishana pete na Richard Fabian
anayeshtakiwa kwa kosa la mtandao kwa kusambaza video za tukio hilo kwenye
mitandao ya kijamii.
Katika uamuzi wake,
Hakimu Chuma amesema Mahakama haiwezi kufanyia kazi maelezo na vitu vya mashaka
na uvumi kuwa washtakiwa wanaweza kudhuriwa na jamii iliyochukizwa na kitendo
wanachoshtakiwa nacho.
“Ni uamuzi wa Mahakama
kuwa dhamana ni haki ya washtakiwa na upande wa mashtaka umeshindwa kuwasilisha
hoja za msingi kwa nini wanyimwe dhamana zaidi ya kutoa hoja za hisia kuwa
wakiachiwa watadhuriwa na jamii bila kueleza watadhurikaje na nani haswa atawadhuru,”
amesema Hakimu Chuma katika uamuzi wake
Washtakiwa wameachiwa
kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja
mwenye kitambulisho na barua ya utambulisho kutoka mamlaka inayotambulika
kisheria pamoja na kusaini hati ya dhamana ya Sh6 milioni. Shauri limeahirishwa
hadi Januari 8, mwakani.
No comments:
Post a Comment