Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu
Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imepunguza gharama ya chanjo ya ugonjwa
wa homa ya ini kutoka shilingi 22,000 kufikia shilingi 5,300 ili kusaidia
upatikanaji wa chanjo hiyo katika vituo vingi vya tiba hapa nchini hususani
vituo vya Umma.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy
Mwalimu katika maadhimisho ya siku ya homa ini
Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka Julai 28 kama ilivyopendekezwa
na Shirika la Afya Duniani (WHO) Kwa lengo la kuelimisha jamii na
kutambua athari za ugonjwa huo.
Ummy amesema kuwa Serikali imeamua kununua dawa ya chanjo ya
ugonjwa huo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kuwawezesha Wananchi
kuipata kwa gharama nafuu zaidi kwa lengo la kuunga mkono kauli mbiu
ya maadhimisho ya ugonjwa huo kwa mwaka huu ambayo inasema “Tokomeza Homa ya
Ini (Eliminate Hepatitis)”.
“Matibabu ya homa ya ini yana gharama kubwa, ambapo kwa mgonjwa
aliyepata maambukizi ya virusi C anaweza kutibiwa kwa millioni tatu hadi tano
kulingana na muda wa tiba ndio maana tunasema bora kinga kuliko tiba,” alisema
Ummy.
Aliongeza kuwa chanjo inayotolewa
nchini kwa sasa ni ya virusi B inayojulikana
kama Hepatitis B japo chanjo ya virusi A ipo na inatolewa nchi
nyingine kutokana na Tanzania kukabiliwa na aina
mbili tu virusi ambavyo ni virusi B na C.
“Kwa sasa hakuna ushahidi wa mlipuko wa homa ya Ini nchini, hata
hivyo wananchi wa Tanzania na Afrika Mashariki wapo katika hatari ya kupata
ugonjwa huu kutokana na njia za maambukizi kufanana kwa kiasi na zile za
maambukizi ya virusi vya ukimwi,” aliongeza Ummy.
Waziri huyo alisema kuwa chanjo hiyo ilianza kutolewa
bure nchini kwa watoto waliozaliwa kuanzia mwaka 2003 na kuendelea. Aidha mwaka
2015 zaidi ya dozi 650,000 ilitolewa kwa watumishi wa afya ili kuwakinga na
hatari ya maambukizi ya ugonjwa huo wakati wakitekeleza
majukumu yao ya utoaji huduma kwa waathirika wa ugonjwa huo.
“Kwa sasa tunaangalia ni namna gani tunaweza kuifikia jamii
iliyobaki ili tuweze kuwapatia chanjo, Serikali imeshafanya mchanganuo rasmi
ambao umeonyesha kiasi cha gharama ya chanjo, vitendanishi vya vipimo vya
awali, kutunza chanjo, kusambaza chanjo na shughuli yenyewe ya uchanjaji,”
alifafanua Ummy.
Aidha amesema kuwa kwa sasa chanjo hiyo inatolewa kwa malipo ya
shillingi 50,000 mpaka 70,000 kwa dozi moja katika baadhi ya vituo
binafsi vya Afya ikiwa ni pamoja na Premier Care Clinic,
IST Na Hindu Mandal kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Ummy amewataka wananchi kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa huo
kwa kuachana na matumizi ya dawa kiholela, vilevi kupita kiasi, madawa ya
kulevya, matumizi ya sindano zisizo salama na vihatarishi vyote vya maambukizi
ya ukimwi kwani wagonjwa wa ukimwi wapo kwenye hatari kubwa ya kupata
maambukizi kuliko wazima.
No comments:
Post a Comment