Serikali imemshauri
Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Tundu Lissu kutekeleza wajibu wake kwa kusimamia weledi akiwa kama
Wakili wa Mahakama Kuu badala ya kufanya Propaganda kwa kutumia lugha ya
kejeli, kuudhi na uchochezi kuituhumnu Serikali kuwa inabana demokrasia nchini.
Hayo yameelezwa leo,
Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu
wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi katika taarifa kwa Umma aliyoitoa juu ya
ufafanuzi kuhusu propaganda na upotoshaji wa Mbunge huyo.
“Vyombo mbalimbali vya
habari leo vimemnukuu Mbunge wa Singida Mashariki Ndugu Tundu Lissu ambapo
pamoja na mambo mengine, huku wakati fulani akitumia lugha za kuudhi, uchochezi
na kejeli, ameituhumu Serikali kuwa inabana demokrasia nchini,” imefafanua taarifa
hiyo.
Taarifa hiyo imesema
kuwa madai kwamba Serikali inakandamiza demokrasia ni propaganda tu za kisiasa,
kutokana na Lissu kuonekana kuchanganya kati ya haki katika demokrasia ambazo
hata yeye amezitumia kuongea na wanahabari bila tashtiti kwa upande mmoja na
misingi ya wajibu kwa upande mwingine ambayo kila mmoja, iwe Tanzania au
kwingineko duniani, anayo na pale anapoikiuka hatua huchukuliwa.
Dkt. Abbasi amesema
kuwa tofauti na upotoshaji wa Lissu, Tanzania ikiwa nchi kiongozi Afrika na duniani
katika kuenzi demokrasia na kupigania haki, si tu inaendelea kuenzi misingi
hiyo bali pia imechukua hatua za wazi kuhakikisha kuwa misingi hiyo inalindwa
na pale mtu na hata taasisi zinapokiuka basi mkondo wa sheria, jambo muhimu
katika utawala bora, huchukua nafasi yake.
Vile vile ameeleza
kuwa, Tanzania ni ikiwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), hivyo imeridhia
Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 na huwasilisha
taarifa zake za utekelezaji wa demokrasia na haki za binadamu katika Kamisheni
ya UN ya Haki za Binadamu.
Pia ni mwanachama
kiongozi wa Umoja wa Afrika (AU) ambapo imeridhia Mkataba wa Afrika wa Haki za
Binadamu na Watu na ni miongoni mwa nchi za kwanza kabisa Afrika kukubali
kushtakiwa na wananchi wake kwa kuridhia itifaki ya Mahakama ya Afrika ya Haki
za Binadamu na pia kukubali kufanyiwa ukaguzi katika utawala bora kupitia
Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
“Ni kwa sababu hizi
basi tunamuasa Ndugu Lissu na wananchi kwa ujumla kujiepusha na propaganda,
kejeli na uzushi usio na msingi dhidi ya Serikali au taasisi zake na pale
ambapo wanadhani kuna haki zimekiukwa badala ya kuvunja sheria ni vyema
kutafuta haki kupitia mkondo wa kisheria ambao tumeuainisha hapo juu,”
imefafanua taarifa hiyo.
Dkt. Abbasi amesema
kuwa Serikali itaendelea kuenzi na kuilinda misingi ya demokrasia, uhuru wa
watu na kuwapa fursa wananchi kushiriki katika uchumi wa nchi hasa wakati huu
wa mageuzi makubwa ya kiutendaji chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli lakini
haitavumilia mtu yeyote au kikundi chochote kitakachojaribu kutumia uhuru
wowote vibaya ili tu kukwaza azma hiyo ya Taifa.
No comments:
Post a Comment