Tuesday 26 September 2017

WAZIRI MWAKYEMBE AZINDUA MPANGO WA USAJILI NA UTOAJI VYETI KWA WATOTO WALIO CHINI YA UMRI MIAKA 5 MTWARA NA LINDI




Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akikata utepe katika Kitabu cha Usajili pamoja na Simu kuashiria Uzinduzi wa Mpango wa Usajili na Utoaji Vyeti kwa Watoto waliochini ya Umri Miaka Mitano kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara leo 26 Septemba, 2017. 


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (aliyevaa kofia ya pama) akiwakabidhi vyeti Wazazi kwa niaba ya watoto wao wenye umri chini ya miaka mitano wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Usajili na Utoaji Vyeti kwa Watoto waliochini ya Umri Miaka Mitano leo Wilayani Tandahimba, Mkoani Mtwara 26 Septemba, 2017.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa katika picha ya pamoja na Wadau mbalimbali wanaosaidia Mpango wa Usajili na Utoaji Vyeti kwa Watoto waliochini ya Umri Miaka Mitano mara baada ya kuuzindua leo Wialayani Tandahimba, Mkoani Mtwara, 26 Septemba, 2017.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. John Palamagamba amezindua Mpango wa Usajili na Utoaji Vyeti kwa Watoto waliochini ya Umri Miaka Mitano kwa Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Uzinduzi huo umefanyika leo katika Viwanja vya Matogolo Wilayani Tandahimba Mkoani Mtwara ukiwa na lengo la kuwasajili watoto waliochini ya umri miaka mitano pamoja na kuwapatia vyeti ambavyo vitawasaidia kutambulika kwao na kisha kupewa nyaraka za uthibitisho yaani  vyeti vya kuzaliwa.

Waziri Mwakyembe amesema kwamba, katika kupanga maendeleo ya nchi kunahitajika takwimu sahihi za matukio muhimu za Watanzania ambazo zinaelezea taarifa zao za kuzaliwa ikiwemo za vifo kwakuwa takwimu hizo zinasaidia kujua mahitaji ya wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, lishe pamoja na sehemu nyinginezo.

“Mpango huu utaondoa utegemezi wa takwimu za kuhisia, takwimu za kukadilia ndugu zangu mfumo tulionao sasa unategemea Sensa ambayo hufanyika kila baada ya miaka 10, na matukio bado yanatokea, hivyo kutumia Mpango huu kutasaidia kupata takwimu sahihi na halisi za Watanzania wote”, alisema, Dkt. Mwakyembe.

Ameongeza kuwa, Mikoa ya Lindi na Mtwara itanufaika na mpango huo kwakuwa Serikali itakuwa inatambua mahitaji halisi ya wananchi kupitia taarifa zitakazochukuliwa za uandikishaji wa watoto hao, huku akisisitiza kuwa, anaamini kwamba mikoa hiyo itakuwa chachu ya kuongezeka kwa idadi ya watoto watakaoandikishwa kama ilivyofanyika katika baadhi ya mikoa mingine ya Tanzania.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome amesema kwamba kama Wizara wana wajibu wa kufikisha huduma hiyo kwa wananchi hususani kwa wananchi ambao wako maeneo ya mbalibila kujali hali yao ya kimaisha huku akisisitiza kwamba kila mtoto atapatiwa haki hiyo ya kuandikishwa na kupewa cheti hivyo.

“Kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano ana haki ya Kikatiba ya kupewa huduma hii, hivyo tutahakikisha kwamba kila mtoto katika Taifa letu anapewa huduma hii bure kupitia RITA”, alisema Prof. Mchome.

Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Bibi Emmy Huddson amesema kwamba,  mpango huo umeanza kutekelezwa leo katika mikoa hiyo miwili ikiwa ni mwanzo wa utatuzi wa changamoto ya upatikanaji wa haki ya mtoto ya kutambuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 pamoja na Mikataba mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda ambayo Tanzania kama nchi imeiridhia.

Amebainisha kuwa, mpango huo haumaanishi kwamba hapo awali huduma hiyo ilikuwa haitolewa isipokuwa huduma hiyo ilikuwa inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutofika kwa huduma hiyo kwa wakati jambo lililosababisha watoto wengi kutosajaliwa kwa watoto na kupatiwa vyeti vyao vya kuzaliwa kwa wakati.

“Kupitia huduma hii, watoto wataweza kupata uthibitisho wa tukio la kizazi au cheti cha kuzaliwa ambacho ni nyaraka muhimu inayomwezesha mtoto kupata huduma mbalimbali kama nchini kama vile ajira, afya, elimu pamoja na huduma na nyinginezo, niwaase wakazi wa Mtwara na Lindi kutumia vyeti hivyo badala ya kutumia Viapo au maelezo ya mdomo”, alisema Bibi Emmy.

Mpango wa Usajili na Utoaji Vyeti kwa Watoto waliochini ya Umri Miaka Mitano nchini unatekelezwa na Ofisi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambao unasimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria, ambapo hapo awali ulianza kutekelezwa katika mkoa wa Dar es Salaam na baadaye ikafuata mikoa ya Mbeya, Mwanza, Iringa, Njombe, Geita, Shinyanga ambapo hivi leo mikoa ya Mtwara na Lindi inajumlisha idadi ya mikoa kufikia tisa.


No comments:

Post a Comment