Tuesday 26 September 2017

JICA YAPONGEZWA KWA KUDUMISHA USHIRIKIANO NA TANZANIA










Serikali imelipongeza Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa ushirikiano wake na Tanzania katika  miradi mbalimbali ya maendeleo hasa katika sekta za Kilimo Afya na Maendeleo ya Jamii kwa kutumia wataalam na uzoefu kutoka Japan.
Pongezi hizo zimetolewa Jijini Dar es Salaam leo na Mkurugenzi Msaidizi wa ushirikiano wa kiufundi kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw.Msafiri Marwa alipokuwa akiwaaga vijana  wa kijapani waliokuwa wanajitolea  katika sekta ya Kilimo na Maendeleo ya jamii hapa nchini.

“Serikali ya Japan kupitia shirika lake la JICA imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na serikali ya Tanzania katika sekta mbalimbali kama vile kuwajengea uwezo Watanzania kupitia ufadhili wa masomo ya elimu ya juu nchini Japan na kuleta watu wa kujitolea katika miradi ya maendeleo hapa nchini,” alieleza Bw. Marwa.

Aidha, Bw.Marwa ambaye alimuwakilisha Naibu Katibu Mkuu Utumishi Bi. Suzani Mlawi aliipongeza Japan kwa kutumia rasilimali watu pamoja na rasilimali fedha kupitia JICA kufadhili utoaji wa huduma za kijamii jambo ambalo ni kipimo cha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.

Amewapongeza vijana wa kijapan kwa kazi nzuri waliyoifanya hapa nchini katika kipindi chote cha miaka miwili ya kuwahudumia watanzania hasa katika sekta ya Kilimo na Afya.

Kwa niaba ya serikali niwapongeze vijana wote mliokuja hapa nchini kwa kufanya kazi na jamii ya Watanzania, mmefanya kazi kwa jitihada kubwa wakati mwingine katika  mazingira magumu, niwahakikishie kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kuimarisha mazingira ya ushirikiano ili kuendeleza uhusiano ” alifafanua Marwa.

Mkurugenzi huyo pia aliwakumbusha vijana hao kuwa mabalozi wazuri nchini Japani na mataifa mengine watakayokwenda ili kuwavutiwa wawekezaji na watalii kuja kuwekeza katika shughuli za maendeleo pamoja na kuleta watalii wengi kwani Tanzania ina vivutio vingi vya utalii, mazingira rafiki kwa wageni na amani ya kutosha.


Kwa upande wake, Mratibu wa kundi la vijana  wa kujitolea kutoka JICA Bw.Ichiro Owa alisema kuwa, anaipongeza serikali ya Tanzania kwa kuwapokea na kuwapa ushirikiano na ulinzi wa kutosha vijana waliokuja kujitolea katika shughuli za maendeleo kwa siku zote ambazo wamekuwa hapa nchini.

“Mpango wetu kwa sasa ni kuleta vijana wengi zaidi wa kujitolea kwasababu ya ushirikiano tulioupata kutoka kwa serikali ya Tanzania ni mzuri  kwani tumefurahia usalama amani na utulivu pamoja na ukarimu wa watanzania ” alifafanua Bw. Owa.

Mratibu huyo wa vijana wa kujitolea kutoka Japan alisema ushirikiano kati ya nchi yake na Tanzania ni wa kihistoria na umekuwa wa manufaa kwa pande zote mbili, aliongeza kuwa  kwa mwaka huu, JICA ina jumla ya vijana 40 wanaojitolea na matarajio yao ni kuongeza vijana  kati ya 60 hadi 70 kwa mwaka ujao.

Vijana wa kujitolea walioagwa katika hafla hiyo ni pamoja na Kyoko Tada aliyekuwa akifanya kazi ya Uuguzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Shu Sato aliyekuwa  katika Ofisi ya Kilimo Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro na Yusuke Sakakibara aliyekuwa anafanya kazi ya maendeleo ya jamii katika Wilaya ya Masasi.


JICA ilianza mpango wake wa kuleta vijana wa kujitolea katika shughuli mbalimbali za maendeleo  mwaka 1967 ambapo takwimu zinaonyesha  kuwa tangu kuja kwa kundi la kwanza    kutoka Japani idadi  imeongezeka  kufikia  vijana 1,568.

No comments:

Post a Comment