Monday 25 September 2017

KAMATI YA UJENZI SHULE YA MSINGI BARIADI YAKAMATWA KWA UBADHIRIFU WA MIL 4.8



Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya kukamatwa kwa kamati ya Ujenzi wa vyoo vya shule ya msingi Bariadi baada ya kutafuna mil 4.8 


Vyoo vya awali vya shule ya msingi Bariadi.


Mkuu wa shule ya Msingi Bariadi Mayila Ndalahwa akihojiwa   na waandishi wa habari juu ya sakata la vyoo na uhitaji kwa wananfunzi wa shule hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, Festo Kiswaga ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kuwakamata na kuwaweka rumande watu watano ambao ni Kamati ya Ujenzi ya Shule ya Msingi Bariadi, baada ya kudaiwa kutumia vibaya fedha za ujenzi wa matundu 14 ya vyoo vya shule hiyo zilizotokana na michango ya wananchi.
Kamati hiyo inadaiwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 4.8 ambazo zilichangwa na wananchi kwa ajili ya ujenzi huo ili kupunguza uhaba wa matundu ya vyoo uliokuwa unaikabili shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 1373.

Kiswaga aliwataja waliokamatwa kuwa ni Mlela Hosea mwenyekiti wa kamati ya ujenzi, Lucas Gervas Makamu Mwenyekiti, Kenedy
Machume, Wodya Husein na Suzan Ezekiel ambao ni  wajumbe wa kamati hiyo.

Kiswaga aliwaonya wote wenye tabia ya kugusa fedha zinatokana na michango ya wananchi kuwa serikali yake itawashughulikia ipasavyo kwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani, na kuwataka wananchi waendelee kuchangia fedha kwa ajili ya kujiletea maendeleo.


 Akizungumzia suala hiyo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bariadi Mayila Ndalahwa anasema dalili za wajumbe hao kufuja fedha zilizochangwa na wananchi kwa ajili ya ujenzi wa vyoo zilianza kuonekana mapema baada ya kumfukuza fundi aliyekuwa ameidhinishwa na mkutano mkuu wa wazazi.

’Kila mzazi alichangia Elfu 7600 ili kufanikisha ujenzi huo, na kamati hiyo ilitokana na wazazi wenyewe…ilionekana walianza kununua vifaa hewa kwa sababu walikuwa wakichukua fedha nyingi lakini wanaleta vifaa vichache, mfano saruji’’ alisema Ndalahwa.

Wanafunzi wa darasa la sita Anastazia Pius na Emanuel Amos walisema wamekuwa wakikutana na foleni kubwa chooni kutokana na msongamano mkubwa wa wanafunzi sabau ya upungufu wa vyoo kwa sababu wanafunzi ni wengi tofauti na mahitaji ya vyoo.

Mmoja wa wazazi aliyekuwa Shuleni hapo Mathias Sakagoi alisema kuwa walichangia ujenzi huo tangu mwezi February lakini hadi sasa umesimama bila taarifa na hali iliyoawasababisha kutohudhuria vikao vya shule baada ya kubaini ubadhirifu uliokuwa ukifanyika.

Shule ya msingi Bariadi ina jumla ya wanafunzi 1373, ina matundu 12, na upungufu wa matundu 57 kwa sasa inakabiliwa na tatizo la uhaba wa matundu ya vyoo kwa muda mrefu ambapo wazazi waliamua kuchangia ujenzi huo ili kuwanusuru wanafunzi hao.


No comments:

Post a Comment