Friday 7 October 2016

WALIOMPIGA MWANAFUNZI MBEYA DAY WAFUKUZWA CHUO



Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof. Joyce Ndalichako




Waziri wa TAMISEMI George Simbachawene 
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof. Joyce Ndalichako ametangaza kuwafukuza chuo walimu wanafunzi walioshiriki kitendo cha kumpiga mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya kutwa ya sekondari mkoani Mbeya.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Waziri Ndalichako amesema kuwa kitendo hicho ni cha kikatili, jinai na walimu hao wanafunzi hawafai kuendelea na taaluma hiyo ya ualimu na kuwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea kuchukuliwa.

Waziri Ndalichako amesema kwa mujibu wa taratibu za vyuo vikuu kitendo kilichofanyika ni kosa la jinai na kuwa hakiwezi kufumbiwa macho.

Waziri pia ametoa onyo kali kwa wanafunzi wanaokwenda kwenye mazoezi kwa vitendo na kuwa kwenda kinyume na taaluma mwanafunzi wa vitendo anakuwa amepoteza sifa, hivyo amewataka kuzingatia maadili ya fani na taaluma wanazozisomea.

Katika hatua nyingine, Waziri wa TAMISEMI George Simbachawene ametangaza kumvua madaraka Mkuu wa Sekondari ya Mbeya Kutwa kwa kufumbia macho ukatili dhidi ya mwanafunzi.

Simbachawene amesema kuwa tukio hilo lilitokea tarehe 28.09.2016 ambapo walimu wa mazoezi kutoka chuo kikuu cha elimu Dar es salaam DUCE na walimu wenzao wa mazoezi kutoka chuo kikuu cha kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere walishirikiana kumwadhibu mwanafunzi wa kidato cha tatu Sebastian Chingulu kwa maelezo kwambza aligoma kufanya adhabu alizopewa na mwalimu Frank Msigwa .

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Simachawene amewataja walimu hao kuwa ni pamoja na

(i) Frank Msigwa - Ndiye aliyesababisha tukio hilo pia ndiye aliyempiga zaidi, huyu anatoka DUCE
(ii) John Deo – Anatoka DUCE
(iii) Sante Gwamoka – Anatoka DUCE
(iv) Evans Sanga – Anatoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

Amesema kuwa baada ya kuona tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii, ofisi yake ilifuatilia na kuamua kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kuagiza mamlaka husika kumvua madaraka mkuu huyo wa shule Magreth Haule .

Sehemu ya taarifa ya Waziri inasema kama ifuatavyo:-
"Nilimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwenda na Vyombo vyake vya ulinzi na Usalama kwenda na kwamba mahojiano kati ya walimu na polisi yanaendelea

Kwa kuwa waliotenda tukio hilo wametoweka tangu tar 29 Sept 2016 na hawajulikanai walipo, nimesikitishwa na kitendo cha Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo kutochukua hatua yoyote ikiwa ni pamoja na kutotoa taarifa hadi leo tulipoona kwenye mitandao ya kijamii, hii ni dalili ya kuwepo kwa dalili ya kulitaka kulificha
Naagiza mamlaka yake ya nidhamu kumvua madaraka mkuu huyo wa shule".

No comments:

Post a Comment