Friday 28 October 2016

SHULE YA MSINGI BUTWA HAINA WALIMU WA KIKE



Shule  ya msingi Butwa iliyopo katika kijiji hicho ndani ya  kisiwa cha Izumacheli ziwa Victoria upande wa Wilaya ya Geita inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu wanawake,  jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya elimu kwa mtoto wa kike.
Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1983 na sasa ina umri wa miaka 33 ikiwa ni shule ya pili katika kata ya Izumacheli, imefahamika kuwa walimu wa jinsia hiyo wanapopangiwa kuripoti maeneo hayo wamekuwa waonga wa kuishi kutokana na mazingira kuwa magumu kwao.

Leticia Zakayo ni mwanafunzi darasa la sita, ni msichana pekee aliyethubutu kupaza sauti yake kwa niaba ya wenzake akiiomba serikali kutatua changamoto ya walimu wa kike shuleni hapo.

‘’Mimi ni mwanafunzi wa darasa la sita tangu nianze masomo yangu shuleni hapa sijawahi kumuona mwalimu wa kike..watoto wa kike tunakabiliwa na changamoto nyingi sana mmoja wetu anapougua tunashindwa kuwaelezea matatizo yetu hawa walimu wa kiume…kama mnavyojua tunakabiliwa na changamoto nyingi,’’alisema Leticia zakayo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Omary Shabani aliangazia  changamoto zinazowakabili watoto, ambapo alisema kuwa mtoto wa kike anapopata matatizo wamekuwa na utaratibu wa kusaidiana wao kwa wao.

 “Ni kweli changamoto hii imekuwepo kwa muda mrefu ni wakati wa serikali kulitizama hili kwa mapana yake watoto hawa hawako huru sana pindi wanapopatwa na shida, wanapokumbana na changamoto tumekuwa tukiwatafuta wanafunzi wakubwa wanasaidiana,’’alisea mwalimu Mkuu.


Mwalimu Herman Kapufi ni mkuu wa Wilaya ya Geita wa kwanza kuitembelea shule hiyo tangu ilipoanzishwa miaka 33 iliyopita ambapo katika ziara yake alipoitembelea jana alikumbana na changamoto hiyo na kuahidi kuwa kufikia januari mwakani shule hiyo itakuwa na walimu wa kike.

No comments:

Post a Comment