Tuesday 16 May 2017

"KAHAWA NA MIWA IWE MKOMBOZI KWA WAKULIMA" - DC KAPUFI



Mkuu wa wilaya ya Geita Mheshimiwa Herman Clement Kapufi amewashauri wananchi wa Wilaya ya Geita kuwekeza nguvu zao katika kilimo cha mazao ya Kahawa na miwa ya sukari ambayo yameonekana yanastawi vizuri katika ukanda wa ziwa viktoria
Mwl. Kapufi ametoa ushauri huo wakati alipofanya  ziara ya kikazi kwa kuwatembelea wakulima wa mazao hayo ambao wameamua kuingia katika kilimo hicho kufuatia ushauri waliopata kutoka kwa wataalamu wa kilimo kutoka Halmashauri kwa kushirikiana na bodi ya sukari Tanzania pamoja na wataalamu kutoka Maruku mkoani Kagera.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia idara ya Kilimo na Umwagiliaji imeamua kuanzisha kilimo cha mazao ya Kahawa na Miwa ambayo hayakupewa kipaumbele hapo awali kwenye wilaya hiyo. 
Kufikia msimu wa kilimo wa 2014/2015 jumla ya miche ya mibuni 41,808 ya kutosheleza hekta 8.6 ambazo ni sawa na ekari 33.2 kati ya lengo la hekta 49 zilisambazwa na kupandwa katika mashamba ya wakulima kwa kata za Nzera,Lwezera,Kakubilo,Nkome,Nyamboge,Senga,Nyamwilolelwa,Chigunga,Bukondo na Nyakagomba ambazo zina hali nzuri ya hewa inayostahimili kustawi vyema kwa kilimo cha kahawa.
 Upande wa kilimo cha miwa kilianzishwa mwaka 2015 na jumla ya ekari 75.5 zimelimwa katika maeneo ya Nzera, Lwezera, Chigunga na Nyamwilololwa kwa ufadhili wa bodi ya sukari Tanzania. 
Miwa hiyo hukomaa baada ya miezi minane 8 na uzalishaji wake kwa ekari moja ni tani 40 kama imetunzwa vyema na baada ya uzalishwaji inatarajiwa kuuzwa kwa bei ya shilingi 60,000/= kwa tani. 
Akiongea na waandishi wa habari na wataalamu ambao alifuatana nao katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Geita Mh Herman Clement Kapufi amesema yuko tayari kuwasaidia wakulima wa Kahawa ambao atahakikisha wanapata mafunzo bora ya kilimo hicho na linakua ni zao mmbadala la biashara kwa wakulima wa Geita badala ya kutegemea dhahabu pekee na kwamba wajue pia hata kilimo ni utajiri. 
Kwa Upande wa afisa kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita anayeshughulikia mazao ya biashara ndugu Samwel Abuya amesema kwa msimu wa kilimo wa wa mwaka 2015/2016 jumla ya tani 5.5 sawa na kilo 5,500 zenye thamani ya shilingi za Kitanzania 8,800,000/= zilizalishwa na wakulima wa zao hilo kwa Halmashauri ya wilaya ya Geita pia kuna wakulima wengine 530 ambao wamehamasika kupanda zao la kahawa na tayari wamejiandikisha kupata miche hiyo ili waweze kujiunga kwenye zao hilo la biashara.


No comments:

Post a Comment