Tuesday 22 August 2017

WADAU WA ZAO LA PAMBA WAKUTANA NA KUJADILI MBINU ZA KUBORESHA ZAO HILO MKOANI GEITA




Wakuu wa Wilaya zilizopo Mkoani Geita pamoja na wabunge na wadau wa Kilimo cha Pamba wakifuatilia kwa makini Mkutano  huo


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe ,Dionis Myinga akijitambulisha mbele ya wadau wa sekta ya kilimo cha pamba.


Mkuu wa Mkoa wa Geita,Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga akizungumza  kwenye mkutano wa wadau wa kilimo cha pamba
Zao la biashara la pamba ni moja kati ya muhimili mkubwa wa uchumi nchini na katika Mkoa wa Geita lakini kwa miaka ya hivi karibuni limeendelea kupoteza umaarufu kutokana na mbegu kutokuwa na ubora pamoja na viuatilifu na bei kutokuwa na mpangilio.

Hali hii ndio inayosababisha wadau wa pamba wakiwemo Viongozi wa Wilaya,Wabunge ,maafisa Kilimo,washauri na wakulima kukutana kwenye ukumbi wa ofisi za Mkuu wa mkoa wa Geita kujadili namna wanavyoweza kuendelea kuinua kilimo cha pamba ili kuwa na faida kwa mkulima na mnunuzi.

Katika Mkutano huo Mgeni Rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Geita,Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga amesisitiza kwa wadau wa kilimo cha pamba kuwa kila mmoja anawajibu wa kuhakikisha kuwa kilimo hicho kinarudi na kinafufuliwa katika ubora wake uliokuwepo miaka ya nyuma.

“Tunawajibu wa kuhakikisha kwamba kilimo hiki kinarudi kwenye ubora wake na hakuna kinachoshindikana ni sisi kujipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kurejea historia kwani itatusaidia”Alisema Kyunga.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe,Safari Nicas Mayala,ameelezea sababu za zao la pamba kuanguka ni kukosa mtu anayeweza kuhudumia na kwamba zamani vyama vya ushirika vilikuwa makini katika usambazaji wa mbegu zenye uhakika.

“Pamba imeanguka baada ya kukosa mtu wa kuihudumia, mtu wa kuhihudumia alikuwa ni ushirika vyama vya ushirika hadi miaka ya 1990, sasa hivi wangekuwa wamesambaza mbegu ya pamba na dawa na Siyodani na ndio maana hapa mkulima amesema kwamba turudishie Siyodani namba 25 ilikuwa inafanya kazi vizuri licha ya kupingwa marufuku kutokana na uharibifu wa mazingira”Alisisitiza Mayala.

Akifunga Mkutano huo Mkuu wa Mkoa Ezekiel Kyunga,amesisitiza kuwa suala la umoja wa wanunuzi wa zao la Pamba, UMWAPA halipo kwani walipatiwa ridhaa ya mwaka mmoja kama majaribio na Waziri ambaye alikuwa madarakani kwa miaka hiyo na kwamba walipatiwa wafanye kazi kwa majaribio kwa mwaka mmoja  na wameshapatiwa maelekezo ya kutowakandamiza wakulima kupitia UMWAPA.


No comments:

Post a Comment