Thursday 24 August 2017

FAMILIA YAGOMA KUMZIKA ANAYEDAIWA KUUAWA MGODINI GGM


Maeneo ya mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM)Shughuli zikiendelea za uchimbaji madini ya dhahabu.

Familia ya kijana Shija Charles mwenye umri wa miaka 25 imegoma kumzika ndugu yao huyo wanayedai kuwa amefariki baada ya kupigwa na walinzi wa mgodi wa dhahabu wa GGM na kutaka uchunguzi wa kina ufanyike.
Tukio la kuuawa kwa kijana huyo limetokea juzi Majira ya saa moja usiku wakati akiwa na wenzake wawili walipoingia kwenye mgodi huo kwa madai ya kwenda kuchukua Mawe ambayo yanajulikana kwa jina la Magwangala.

Vijana walionusurika kwenye tukio hilo Filipo Enock na Shija Mashemba wamesema waliingia kwenye eneo la mgodi kwenye eneo la Piti na wakati wanateremka kwenye maeneo ya barabara ya mgodi walikutana na walinzi  na kwamba mwenzao alikamatwa wakati wakikimbia .

Mwenyekiti wa Mtaa wa Elimu kata ya Nyankumbu alikokuwa akiishi kijana aliyeuawa Bw Hassan Mshora Malima amesema baada ya kupata taarifa za kifo hicho walifika kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Mkoa wa Geita na kukuta mwili wa marehemu ukiwa na majeraha ya kupigwa.

Msemaji wa Familia ya kijana huyo Bw Kazimili Malole amesema hawako tayari kuchukua mwili huo kwa ajili ya maziko hadi watakapopata ukweli wa kifo chake.

“Sisi  kama familia hatupo tayari kuchukua mwili wa marehemu hadi pale uchunguzi utakapo fanyika kujua ndugu yetu ni kipi ambacho kimepelekea kuondoa uhai wake na tunaomba serikali itusaidie kwa swala hili tupate haki zetu za msingi”Alisema Kazimilia.

Meneja mahusiano ya jamii wa Mgodi huo Bw Manase Ndoroma amekanusha taarifa za kupigwa kwa kijana huyo hadi kufariki na kwamba alianguka kwenye shimo mgodini na kwamba viongozi wa jadi waliitwa kushuhudia tukio hilo.

“Mgodini ndani kuna mashimo ambayo huwa tunachimba na kuyaacha wazi watu wamekuwa wakiingia kinyemela kwenye maeneo hayo ambayo ni hatarishi kwa maisha yao na mwisho wa siku wengi huanguka na kupoteza maisha kutokana na maeneo hayo kuwa na mwamba mkali,na sisi tumekwisha kusema kama kuna mwananchi anahitaji kuja mgodini kwa ajili ya kuona shughuli za uchimbaji  ni vyema wakafuata utaratibu kuliko kuingia kinyemela kwani kuna maeneo ambayo ni hatarishi”Alisema Manase.


Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoani Geita  Mponjoli Mwabulambo  alipotafutwa kwa njia ya simu amesema hayupo ofisini kwa muda huo na yupo kwenye oparesheni na anatarajia kufika jioni ofisini kwake.

No comments:

Post a Comment