Friday 23 December 2016

SUMATRA YAUNDA KIKOSI KAZI KUDHIBITI UPANDISHAJI HOLELA WA NAULI KIPINDI CHA SIKUKUU ZA MWISHO WA MWAKA



Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) imeunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kudhibiti upandashaji holela wa  nauli kwa mabasi yaendayo mikoani wakati wa kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka.
Hayo yamesemwa jana na Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo David Mziray wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari  hii, akieleza namna mamlaka hiyo inavyodhibiti upandaji wa nauli za mabasi yaendayo mikoani.

“Kuna timu ambazo ziko katika vituo vyote vya mabasi makubwa katika kila mkoa, timu hizo zinathibiti masuala ya nauli, usalama wa magari , kuhakikisha leseni za mabasi pamoja na muda uliopangiwa kuondoka vituoni,” alifafanua Mziray.

Aliongeza kuwa mamlaka hiyo imeruhusu mabasi yanayobeba abiria 40 na kuendelea kuomba leseni za muda  za kusafirisha abiria katika mikoa ambayo ina wasafiri wengi zaidi katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.

Kwa mujibu wa Mziray alisema mabasi hayo yatakuwa yakikaguliwa kwanza ndipo yanapewa leseni za muda pamoja na kupangiwa nauli ambazo watatozwa abiria kutokana na mkoa ambao gari hilo litakwenda.


Akizungumzia kikosi kazi hicho, Mziray alisema kuwa mwanzoni mwa wiki hii timu iliyoko kituo cha mabasi cha Ubungo ilikamata mabasi manne ambayo yalipandisha nauli kwa abiria na kuchukuliwa hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment