Monday 19 March 2018

WANANCHI WA RULEGEA GEITA WAANZA UJENZI WA SHULE KUNUSURU WANAFUNZI KUVUKA MAJI

Baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Rulegea na viongozi wa chama cha mapinduzi(CCM)wilaya ya Geita wakishiriki kuchimba msingi kwaajili ya Ujenzi wa shule ya Msingi Kijijini Hapo.

Mkuu wa wilaya ya Geita Mwl Herman Kapufi (Katikati),Akiwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Geita,Julius Peter(Kushoto)wakisali kwenye makabuli ya watoto watatu ambao walifariki baada ya kuzama na maji wakati wakitokea shule.

Afisa Elimu wa kata ya Izumacheli Bw Thomson Jerusinga,akisoma taarifa ya Ujenzi wa shule hiyo. 

Diwani wa Kata ya Izumacheli, Bw Ismail Manyama  akisisitiza wananchi kushirikiana kwenye shughuli ya Ujenzi wa shule.

Mkuu wa wilaya ya Geita,Mwl Herman Kapufi akiwasisiza wananchi kuwa wamoja na kushirikiana na serikali ili waweze kumaliza ujenzi wa Shule.

Mkuu wa wilaya ya Geita,Mwl Herma Kapufi pamoja na wananchi wakishiriki kuchimba Msingi kwaajili ya ujenzi wa shule.

Kufuatia ajali ya maji iliyosababisha vifo vya wanafunzi watatu (3) wakati wakitoka shuleni mnamo Mei 22 mwaka jana(2017) kitongoji cha Rulegea, kijiji cha Butwa Kata ya Izumacheli wilayani Geita, wananchi wa eneo hilo wameanzisha ujenzi wa shule kwa lengo la kuwaepusha wanafunzi na kusafiri majini umbali mrefu kufuata Elimu.

Katika ujenzi huo wananchi hao wanashirikiana na mkuu wa Wilaya ya Geita Mwl. Herman Kapufi na viongozi wa  chama cha mapinduzi(CCM).
Hatua hiyo inatokana na wanafunzi kuendelea kupata shida ya kuvuka mara kwa mara pindi wanapokwenda na kutoka shuleni kwa kutumia mitumbwi hivyo kuhatarisha maisha yao.

Afisa Elimu wa kata ya Izumacheli Bw Thomson Jerusinga alisema tatizo la watoto kuvuka maji mara kwa mara limesababisha wananchi wengi kuhama kijijini hapo.

“Kabla ya tukio la Mei 22 mwaka jana kitongoji hiki kilikuwa na Kaya 184 lakini baada ya lile tukio la kuzama wanafunzi, wananchi wengi walihama kwa hiyo ikasababisha kuwepo kwa Kaya 60 badala ya mia moja themanini na nne(184). Eneo ambalo tunatarajia kuanza ujenzi litaweza kujenga vyumba vya madarasa pamoja na ofisi za walimu na viwanja vya michezo” Alisema Jerusinga.

Diwani wa Kata hiyo Bw Ismail Manyama alisema wanafunzi wa eneo hilo wameendelea kupata shida kutokana na kuvuka maji hivyo kukamilika kwa shue hiyo kutawasaidia kuepuka kwenda kijiji jirani.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Geita Mwl Herman Kapufi aliwasisitiza wananchi hao kuwa wamoja ili waweze kufanikisha ujenzi huo wa shule pamoja na Nyumba za walimu na kwamba serikali ipo nao bega kwa bega kuhakikisha kwamba wanafanikisha Ujenzi huo.

Nae Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Geita, Bw Barnabas Mapande amewataka wananchi hao kutowasikiliza watu wanaowapotosha katika kushiriki shughuli za maendeleo kwani kufanya hivyo ni kuweka hazina kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.


Baadhi ya wananchi wa eneo hilo wamesema kuna kila sababu ya kushirikiana na viongozi wao kujenga shule hiyo kwa manufaa ya watoto wao


No comments:

Post a Comment