Friday 25 November 2016

WAZIRI WA MICHEZO NAPE NNAUYE AKATAA MAMLUKI SHIMMUTA



Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akizungumza na washiriki wa mashindano ya SHIMMUTA wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo Novemba 24, 2016 yanayofanyika Jijini Tanga


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akicheza muziki aina ya kwaito pamoja na wachezaji na viongozi wa timu shiriki wakati wa sherehe za uzinduzi wa mashindano ya SHIMMUTA yanayofanyika Jijini Tanga

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye amekemea vikali baadhi ya tabia ya viongozi wa timu zinazoshiriki michezo mbalimbali kutumia wachezaji wasiostahili kutumika katika mashindano husika.

Ameyasema hayo wakati akizindua mashindano ya michezo mbalimbali yanayoandaliwa na Shirikisho la Michezo ya mashirika ya Umma na Binafsi (SHIMMUTA) yanayoendelea Jijini Tanga ambayo yameshirikisha timu mbalimbali kutoka mashirika ya Umma na Binafsi Tanzania.

Mhe. Nnauye amewataka viongozi wa SHIMMUTA kufanya uhakiki upya wa wachezaji wa timu shiriki ili kuondoa lawama zinazoweza kutokea na kupata mshindi anayestahili kwa kufata Sheria na taratibu zote za mashindano.

“Nawaomba viongozi muangalie na kupitia upya wachezaji wa timu shiriki ili kusiwe na zengwe lolote katika mashindano haya na mshindi katika kila mchezo apatikane kihalali” alisisitiza Mhe. Nnauye.

Aidha ametoa wito kwa  mashirika kutenga muda na fedha ili kuwezesha timu zao kushiriki katika michezo ikiwa ni moja ya kujenga mshikamano na amani kwa watanzania na pia kujenga afya ya mwili na akili.

Mashindano ya SHIMMUTA yameshirikisha mashirika ya Umma na Binafsi katika michezo 12 ikiwemo Mpira wa Miguu(Football), Mpira wa Pete(Netball),kuvuta kamba, Riadha, Mchezo wa vishale(Darts),Mchezo wa Pooltable, mchezo wa bao, Karata,kukimbia na magunia.



No comments:

Post a Comment