Friday 18 November 2016

TANZANIA KUENDELEA KUSIMAMIA HISTORIA YA UKOMBOZI WA BARA LA AFRIKA





Serikali ya Tanzania itaendelea kuweka historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika kwa kuhifadhi kumbukumbu zote huku ikitunza na kuweka alama maeneo ambayo yalitumika wakati wa kupigania Uhuru wa Bara la Afrika na kutunza makaburi ya wapigania uhuru hao pamoja na kuyafanya kuwa ya kihistoria.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokutana na Waziri wa Utamaduni na Sanaa wa Afrika ya Kusini Mhe.Nathi Mthehwa aliyeko nchini kwa ziara ya siku tatu kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili katika sekta ya Utamaduni na Sanaa.

 “Tumeanza kuandika historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika kwa kuhoji baadhi ya wanaharakati walioshiriki katika kuwasaidia wapigania uhuru kuanzisha vyama vyao vya ukombozi ambapo historia hii itahifadhiwa kwa njia ya sauti na picha lakini pia tutaendelea kutunza kumbukumbu zote tutakazozipata na kuwekea alama maeneo ambayo yalitumika wakati wa kupigania uhuru” amesema Mhe. Nnauye

Aidha, Mhe. Nnauye amesema kuwa makubaliano yaliyosainiwa mwaka 2011 kati ya Tanzania na Afrika ya Kusini kufuta Visa ya kusafiria kati ya nchi hizo mbili yameleta  mabadiliko makubwa katika eneo la Sanaa nchini kwani wasanii wamekua wakitumia fursa hiyo kwenda Afrika ya Kusini kuandaa kazi zao na kuzifanya kuwa na ubora zaidi.

Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni na Sanaa wa Afrika Kusini Mhe. Nathi Mthehwa ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili na kuthamini mchango uliofanywa na Tanzania katika kukomboa nchi ya Afrika ya Kusini.

Pamoja na hayo Mhe. Mthethwa ameahidi kuendeleza ushirikiano ulipo na kuthamini maendeleo yaliyopo kwenye maeneo ya Utamaduni na Sanaa kwa kuhakikisha kuwa mafanikio ya Sekta za Ubunifu ndani ya Afrika ya Kusini yanakua sehemu ya mafanikio ndani ya nchi ya Tanzania.

Ziara hii inaangalia namna nchi hizi mbili zinaweza kuimarisha makubaliano ya mwaka 2011, katika maeneo mengine ya mashirikiano kama vile upande wa tasnia ya filamu ambapo Afrika ya Kusini imekua ikifanya vizuri ikiwemo kusimamia haki za wasanii kwa kutengeneza mifumo ya kisheria ya kulinda haki za ubunifu na kuongeza mahusiano ya  nchi hizo mbili.


Waziri huyo  atatembelea Mkoa wa Morogoro kwenye kambi ya wapigania Uhuru wa Afrika ya Kusini Mazimbu, Dakawa pamoja na Bagamoyo ambapo kulikua na kambi yao,pamoja na baadhi ya maeneo Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment