Wednesday 16 November 2016

ASILIMIA 75 YA WATANZANIA KUNUFAIKA NA HUDUMA YA UMEME IFIKAPO 2025



Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa uboreshaji huduma za Umeme
Serikali imedhamiria kuimarisha mtandao wa usafirishaji na usambazaji umeme nchini ili kufikia malengo ya Taifa ya Asilimia 75 ya watanzania wanaonufaika na huduma ya umeme ifikapo 2025.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa uboreshaji huduma za Umeme Jijini Dar es Salaam wenye lengo la kuboresha usambazaji na usafirishaji wa umeme katika jiji hilo.

Mhe. Majaliwa alisema kuwa Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imekuwa katika jitihada mbalimbali za kuboresha miundombinu yake ili hatimaye huduma hiyo ili iweze kuwafikia wananchi wengi na katika ubora unaohitajika.

“Nimeambiwa kuwa mradi huu wa kuboresha miundombinu ya umeme ulilenga kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme wa uhakika hususani katika jiji la Dar es Salaam, hivyo kukamilika kwa mradi huu kutafungua fursa nyingi za uzalishaji na kupelekea upatikanaji wa fursa za ajira za uhakika kwa wananchi” alifafanua Waziri Mkuu.

Mhe. Majaliwa alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kutekeleza ahadi yake ya  kusambaza na kuwapatia wananchi umeme wa uhakika ili kuweza kufanikisha shughuli za kiuchumi kwa ufanisi na hivyo kuongeza pato la Taifa.

“Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi iliahidi kuendeleza kusambaza umeme wenye uhakika Mijini na Vijijini, hivyo Serikali imara inayojali maslahi ya wananchi wake ni ile inayotoa ahadi na kuzitekeleza” aliongeza Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu alisema kuwa upatikanaji wa Umeme wa uhakika utaiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda ikiwa ni lengo la Serikali ya Awamu ya Tano.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo ameutaka uongozi wa TANESCO kushughulikia na kumaliza changamoto ya kukatika kwa umeme nchini kwani kufikia uchumi wa kati kupitia  viwanda itahitaji umeme wa uhakika.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi. Felchesmi Mramba alisema kuwa Mradi huo umetumia jumla ya Shilingi bilioni 74.6, ikiwa ni  fedha kutoka Serikali ya Finland kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Mhandisi. Mramba aliongeza kuwa Mradi huo utasaidia kuvutia wawekezaji wapya katika Sekta za viwanda na biashara nchini.


Pia Waziri wa Biashara na Maendeleo wa Finland Bw. Kai Mykkanen, alisema kuwa Serikali ya Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala ya maendeleo hususani katika sekta ya Nishati.

No comments:

Post a Comment